AK Yatangaza Tarehe Mpya za Mashindano ya Majaribio ya Riadha Kitaifa
Mashindano ya majaribio ya riadha ya kitaifa ya kuiteua timu itakayoshiriki katika mashindano ya riadha duniani yataandaliwa tarehe 22 mwezi huu, na wala sio tarehe 1 na 2 Agosti kama ilivyotangazwa hapo awali. Mbio hizo zitafanyika katika uwanja wa Ulinzi, na wanariadha walioalikwa pekee ndio watakaoruhusiwa kushiriki, kwa mujibu wa Chama cha Riadha Nchini (AK). Kulingana na taarifa ya AK, mabadiliko hayo ya tarehe yalitokana na kutokuwepo kwa nafasi ya kuandaa mashindano hayo katika uwanja huo. Chama cha riadha nchini kimedokeza kuwa wanariadha walio na muda unaoruhusiwa na ambao wametimiza masharti ya Shirikisho la Kupambana na Matumizi ya Dawa Haramu watakubaliwa kushiriki mashindano hayo. Kenya inatarajiwa kukiteua kikosi thabiti kitakachoshiriki mashindano hayo ya riadha duniani yatakayoandaliwa jijini Tokyo kuanzia Septemba 13 hadi 21 mwaka huu. Kenya itakuwa inaangazia kuboresha matokeo iliyoafikia katika mashindano ya mwaka 2023 yaliyofanyika jijini Budapest, Hungary, ambapo ilimaliza katika nafasi ya tano kwa kujizolea jumla ya nishani 10, Tatu za dhahabu, Tatu za fedha, na Nne za shaba.
Read More