Wakili wa Cardi B Ajibu Kesi ya Kipaza Sauti
Wakili wa rapa kutoka Marekani Cardi B, Drew Findling, ameibuka na kuikosoa vikali kesi mpya ya madai iliyofunguliwa dhidi ya mteja wake, akisema ni jaribio la kutaka kumpora pesa kwa kutumia jina lake maarufu. Kauli ya Findling imekuja kufuatia mwanamke mmoja, anayetambulika kama Jane Doe, kufungua kesi ya madai dhidi ya Cardi B kwa tuhuma za shambulio la mwili, uzembe na dhuluma ya kihisia, akidai kuwa alijeruhiwa baada ya kurushiwa kipaza sauti na rapa huyo wakati wa tamasha la Drai’s Beachclub huko Las Vegas mnamo Agosti 2023. Kwa mujibu wa maelezo ya Jane Doe, Cardi B alikuwa akitumbuiza katika hafla ya mchana iliyokuwa ikifanyika wakati wa joto kali, ambapo aliwaomba mashabiki wamwagie maji ili kupooza. Mwanamke huyo anasema alifanya hivyo kwa nia njema, lakini alichokutana nacho ni kurushiwa kipaza sauti kwa nguvu na Cardi B, kitendo ambacho sasa anadai kilimsababishia madhara ya kimwili na kiakili. Ingawa tukio hilo lilichukua sura kubwa mitandaoni wakati huo, uchunguzi wa polisi haukupelekea kufunguliwa kwa mashtaka yoyote ya jinai dhidi ya Cardi B. Polisi waliamua kufunga jalada hilo baada ya kukosa ushahidi wa kutosha, na kesi hiyo haikuwahi kufika kwa Mwendesha Mashtaka wa Kaunti. Hata hivyo, Jane Doe sasa ameamua kufungua kesi ya madai miaka miwili baadaye, akidai kuwa hata mnada wa kipaza sauti hicho kwa ajili ya shughuli za hisani ulimvuruga kisaikolojia na kumrudisha katika hali ya huzuni aliyoipitia baada ya tukio hilo. Mashabiki wa Cardi B wamejitokeza mitandaoni wakimtetea msanii huyo, wengi wakisema mwanamke huyo alitafuta kiki na sasa anajaribu kutumia tukio la zamani kujinufaisha kifedha. Hadi sasa, Cardi B hajatoa tamko la moja kwa moja kuhusu kesi hiyo mpya, lakini timu yake ya kisheria imeweka wazi kuwa wataipinga vikali hadi mwisho.
Read More