Tokyo 2025: Kipyegon Atetea Ubingwa, Dorcus Ewoi Aipatia Kenya Fedha
Mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia Faith Kipyegon aliendeleza utawala wake katika mbio za mita 1500, aliposhinda taji yake ya nne mfululizo ya dunia katika siku ya nne ya Mashindano ya Riadha ya Dunia jijini Tokyo Japan. Kipyegon ambaye pia ni bingwa mara tatu wa Olimpiki alitumia muda wa dakika 3 na sekunde 52.15 na kujiongeza taji nyingine ya dunia. Alimaliza mbele ya mwenzake Dorcus Ewoi, ambaye alitumia muda wake bora wa dakika 3 na sekunde 54.92 kunyakua fedha, na Jess Hull wa Australia, aliyenyakua shaba kwa dakika 3 na sekunde 55.16. Kipyegon sasa mwanamke wa pili kushinda taji nne ya dunia katika mbio moja baada ya Shelly-Ann Fraser-Pryce ambaye ameshinda taji tano ya mbio za mita 100. Nelly Chepchirchir alimaliza wa nne kwa dakika 3 sekunde 55.25. Wakati huo huo, matumaini ya Kenya ya kunyakua medali zaidi katika Mashindano ya Riadha ya Dunia yaliboreshwa baada ya bingwa wa Olimpiki Emmanuel Wanyonyi na Kelvin Kimtai kufuzu kwa mbio za nusu-fainali ya mbio za mita 800. Kwa sasa Kenya inashikiliaa nafasi ya pili kwenye jedwali ya medali ikiwa na medali tano, 3 za dhahabu na moja ya fedha, nyuma ya Marekani, ambayo inaongoza kwa jumla ya nishani nane, zikiwemo sita za dhahabu.
Read More