Femi One Achoshwa na Wimbi la Wakosoaji Mtandaoni
Msanii wa Hiphop kutoka Kenya, Femi One, ameonyesha kuchoshwa kwake na kile alichokitaja kuwa wimbi la watu mitandaoni wanaojifanya wataalamu wa muziki huku wakitumia muda wao mwingi kuwakosoa wasanii. Kupitia mitandao yake ya kijamii, Femi One amesema kuna kundi la watu wanaoamini kuwa wanaifahamu sekta ya muziki kuliko wasanii wenyewe, jambo analodai linakosa msingi. Kwa mujibu wake, watu hao hutoa ushauri mwingi na hukosoa kila hatua ya wasanii ilhali wao binafsi hawana kazi wala mafanikio ya kujivunia. Msanii huyo ameongeza kuwa ukosoaji wa mara kwa mara usio na mwelekeo wala suluhisho umekuwa kero kubwa, akisisitiza kuwa si kila anayetoa maoni mitandaoni ana uelewa wa kina kuhusu kazi, changamoto na juhudi zinazowekwa katika muziki. Femi One amewataka wakosoaji hao wajikite katika shughuli halali za kuingizia kipato na kujijenga kimaisha badala ya kutumia muda wao mwingi kuwakosoa wasanii kila wakati. Amesisitiza kuwa muziki ni kazi kama kazi nyingine, inayohitaji heshima na kuthaminiwa.
Read More