Mataifa ya Afrika Mashariki Kushirikiana Kiusalama kwa CHAN 2025

Mataifa ya Afrika Mashariki Kushirikiana Kiusalama kwa CHAN 2025

Mataifa ya Afrika Mashariki yameafikiana kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha usalama wakati wa mashindano ya Kombe la Mataifa Bingwa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani ya Nchi (CHAN) yatakayofanyika mwezi ujao. Akizungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hayo, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen alisema kuwa mashauriano ya kina tayari yanaendelea kati ya Kenya, Uganda, na Tanzania, mataifa matatu yatakayoandaa mashindano hayo kwa pamoja ili kuimarisha usalama hasa kwenye maeneo ya mipakani na kuhakikisha usafiri salama wa timu na mashabiki. Murkomen alisisitiza kuwa hatua madhubuti zimewekwa ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa utulivu na bila hitilafu. Alibainisha kuwa udhibiti wa umati wa watu umepewa kipaumbele kikuu, ikizingatiwa kuwa maelfu ya mashabiki, wakiwemo wageni kutoka mataifa jirani, wanatarajiwa kuhudhuria mechi mbalimbali. β€œKuna mifumo ya uangalizi ya kisasa inayowekwa katika viwanja vyote vitakavyotumika, pamoja na itifaki za dharura ili kuhakikisha usalama wa mashabiki na wachezaji,” alisema Murkomen. Mashindano ya CHAN yanatarajiwa kuimarisha mshikamano wa kikanda, si tu kupitia michezo, bali pia kupitia ushirikiano wa kiusalama na maandalizi ya pamoja yanayoakisi uwezo wa Afrika Mashariki kuandaa mashindano ya kimataifa kwa mafanikio.

Read More