Harmonize Atoa Wito kwa Wasanii Watumie Singeli Kuelimisha Jamii
Mwanamuziki nyota kutoka Tanzania, Harmonize, amewataka wasanii kutumia muziki wa Singeli kuibua mijadala ya kijamii na kupeleka ujumbe wenye maana kwa jamii badala ya kuishia kwenye burudani ya kawaida. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize alisema kuwa Singeli ni mtindo wa muziki wenye nguvu kubwa ya ushawishi na unastahili kutumiwa kuelimisha, kukuza maadili, na kuunganisha vizazi vyote kwa ujumbe wake. Harmonize, anayefahamika pia kwa jina la Konde Boy, alisisitiza kuwa kutumia Singeli kwa maudhui ya kijamii kutaongeza thamani ya muziki huo na kuufanya upokelewe na watu wa rika zote, si kundi moja tu. “Singeli ni mziki mkubwa sana. Wasanii tuutumie kuimba mambo ya msingi yenye maana, si kila siku kufurahisha tu,” aliandika msanii huyo katika ujumbe wake uliopata mapokezi makubwa mtandaoni. Katika hatua nyingine, Harmonize alidokeza kuwa anatarajia kuachia nyimbo mbili kubwa za kimataifa (International Bangers) usiku mmoja ndani ya mwezi Julai. Alisema kuwa ngoma hizo zitakuwa za kipekee na atawashirikisha wasanii wawili wakubwa wa kimataifa, ingawa hakuwataja majina yao. Hii imeongeza hamasa miongoni mwa mashabiki wake waliotamani kuona sura mpya ya kimataifa kutoka kwa bosi huyo wa Konde Gang. Singeli kwa sasa ni miongoni mwa mitindo ya muziki inayoshika kasi sana Tanzania. Julai 3, tulishuhudia msanii mkubwa wa Bongo Flava, Alikiba, akiachia wimbo wake wa kwanza wa Singeli uitwao Ubuyu, ambao mbali na kuburudisha, unatoa ujumbe mkali dhidi ya tabia zisizofaa katika jamii. Harmonize amepongeza mwelekeo huo, akiwahimiza wasanii wengine kuiga mfano huo kwa kutumia muziki kama chombo cha kuelimisha, kuonya, na kujenga.
Read More