Nyota Ndogo Akemea Ubaguzi wa Rangi Mitandaoni
Msanii mkongwe wa muziki nchini Kenya, Nyota Ndogo ameonyesha wazi kukerwa na baadhi ya watu wanaoendelea kumkejeli mtandaoni kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Kupitia mitandao yake ya kijamii, amesema kuwa maoni hayo hayamvunji moyo bali yanadhihirisha kiwango cha ujinga na chuki mitandaoni. Nyota Ndogo amesisitiza kuwa rangi yake ya ngozi sio tatizo, bali ni kitu cha kipekee na cha kujivunia. Amesema kuwa rangi ya mtu haiuzwi dukani, na hivyo tofauti za asili hazipaswi kuwa chanzo cha kumdhalilisha yeyote. Msanii huyo, ambaye amekuwa kwenye muziki kwa miaka mingi, amesema ataendelea kupigania heshima na kukemea ubaguzi wa aina yoyote, huku akiwasihi wafuasi wake kujipenda na kukubali muonekano wao bila aibu. Hivi karibuni, msanii huyo alipokea maoni ya kumdhalilisha kutoka kwa mfuasi mmoja aliyedai kuwa shida yake ni kuwa mweusi sana. Kauli hiyo ilizua hisia kali na kuibua mjadala kuhusu ubaguzi wa rangi dhidi ya wasanii na watu mashuhuri mtandaoni.
Read More