Oga Obinna Amuinua Shalikido Kwa Msaada wa Kifedha na Ajira Mpya
Mtangazaji maarufu na mchekeshaji Oga Obinna, amejiunga na orodha ya mastaa ambao wameamua kumsaidia msanii wa muziki wa Gengetone, Shalikido, ambaye hivi karibuni aliomba umma imsaidie kutokana na maisha kumuendea vibaya. Katika hatua ya kuonyesha upendo na mshikamano kwa wasanii wachanga, Oga Obinna ameamua kumpa Shalikido kazi ya mwaka mmoja kama mshawishi wa mitandaoni (influencer), akimwahidi nafasi ya kukuza kipato chake kupitia majukwaa ya kidijitali. Obinna pia ametoa zawadi za vifaa vya nyumbani kwa Shalikido ikiwemo sofa, godoro na zulia, hatua iliyochukuliwa kama ishara ya kumuwezesha kuanza maisha mapya kwa ustawi na heshima. Zaidi ya hayo, kupitia kipindi chake cha moja kwa moja (live show) kwenye YouTube, Oga Obinna alifanikiwa kuchangisha kiasi cha KSh 62,000 kwa ajili ya kumsaidia msanii huyo kijana. Michango hiyo ilitoka kwa wafuasi wake walioguswa na hali ya Shalikido na waliotaka kuona maisha yake yakibadilika. Hatua hii ya Oga Obinna imepongezwa na wengi kama mfano bora wa usaidizi wa kijamii na kuinua vipaji vya vijana, hasa wale wanaokumbwa na changamoto za kiuchumi. Hatua hii ya Obinna inakuja siku chache tu baada ya mchekeshaji mwingine maarufu, Eric Omondi, kumsaidia Shalikido kwa kumpatia pikipiki mpya na mahitaji mengine muhimu ya nyumbani. Msaada huo ulitolewa baada ya Shalikido kufunguka hadharani kuhusu hali ngumu ya maisha aliyokuwa akipitia, hali iliyomlazimu kushindwa hata kumudu mahitaji ya msingi ya familia yake.
Read More