Fik Fameica: Pallaso Ni Shabiki Tu, Si Mlezi Wangu Kimuziki
Mwanamuziki kutoka nchini Uganda Fik Fameica amevunja ukimya na kukanusha vikali madai ya msanii mwenzake Pallaso, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akidai kuwa alihusika pakubwa katika kukuza safari yake ya muziki. Hii ni baada ya Pallaso kudai kuwa alimtoa Fik Fameica kwenye mitaa ya Kawempe, na kumtambulisha kwenye muziki, na hata kumsaidia kifedha alipokuwa anaanza safari yake ya muziki. Hata hivyo, Fik Fameica kwenye mahojiano yake hivi karibuni ameyakana madai hayo akisema kwamba Pallaso hajawahi kutoa mchango wowote wa maana katika mafanikio yake. Alieleza kuwa Pallaso alikuwa tu shabiki kama walivyo mashabiki wake wengine. “Pallaso aliwadanganya. Hajawahi changia chochote katika safari yangu ya muziki. Alikuwa tu shabiki wangu, si zaidi ya hapo,” alisema Fameica katika mahojiano na runinga moja nchini Uganda. Fameica alisisitiza kuwa yeye ni msanii aliyejijenga mwenyewe (self-made), na kwamba mafanikio yake yalianza mara ya kwanza tu alipoingia studio. “Mimi ni msanii aliyejijenga. Mara ya kwanza niliingia studio, nilitoa kibao ‘Pistol’ ambacho kilipokelewa vizuri,” aliongeza. Fik Fameica alipata umaarufu mkubwa mwaka 2018 kupitia wimbo wake maarufu “Kutama”, na tangu wakati huo amekuwa akitoa nyimbo kali mfululizo na kumuweka katika nafasi ya juu kama mmoja wa wasanii bora zaidi katika tasnia ya muziki Afrika Mashariki.
Read More