Rayvanny Aandika Historia Juba, South Sudan kwa Kujaza Uwanja wa Taifa
Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Rayvanny, ameandika historia mpya katika tasnia ya burudani barani Afrika baada ya kufanikisha tamasha kubwa lililovunja rekodi kwa kuhudhuriwa na zaidi ya watu 50,000 katika Uwanja wa Taifa wa Juba, South Sudan. Hili ndilo tamasha la kwanza katika taifa hilo lenye kiingilio rasmi kufikia kiwango hicho cha mahudhurio. Kutokana na mafanikio hayo ya kipekee, Rayvanny alitunukiwa Tuzo Maalum ya Heshima (Sold Out Plaque) kutoka kwa uongozi wa Juba National Stadium kama ishara ya kuthamini mchango wake katika muziki na kuvuka mipaka ya burudani ya Afrika Mashariki hadi Kati. Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Rayvanny alieleza shukrani kwa taifa hilo kwa mapokezi ya kipekee na mafanikio hayo ya kihistoria. “Thanks a lot beautiful country South Sudan. Big thanks to Juba National Stadium for the Sold Out Plaque. Big thanks to all fans for the love and support,” Aliandika kwa hisia. Rayvanny pia alibainisha kuwa hilo ndilo tamasha la kwanza nchini South Sudan lenye kiingilio ambalo limeweza kuvutia hadhira ya zaidi ya watu elfu hamsini. Tamasha hilo linaashiria hatua kubwa kwa Rayvanny, ambaye ameendelea kujizolea sifa kama msanii wa kimataifa mwenye uwezo wa kuvutia mashabiki kwa kiwango kikubwa. Aidha, tukio hilo limedhihirisha jinsi muziki wa Bongo Fleva unavyozidi kupanuka na kukubalika katika nchi mbalimbali za Afrika, ukiwaunganisha watu kupitia ujumbe na burudani ya hali ya juu. Kwa mafanikio haya, Rayvanny amejiweka katika nafasi ya juu miongoni mwa wasanii wanaobadilisha sura ya muziki wa Afrika, akivunja rekodi, kuandika historia, na kuendeleza utambulisho wa sanaa ya Afrika Mashariki kwenye jukwaa la kimataifa. South Sudan, kwa hakika, haitamsahau hivi karibuni.
Read More