Staa wa muziki wa Nigeria, Tiwa Savage, amegusa hisia za mashabiki baada ya kumwaga machozi alipokuwa akitumbuiza wimbo wake Somebody’s Son akishirikiana na Brandy, wakati wa onesho lililofanyika nchini Benin.
Kwa mujibu wa video zinazosambaa mitandaoni, Tiwa alionekana akisimama kwa muda katikati ya uimbaji wake, huku akishindwa kuendelea kuimba kutokana na hisia kali zilizomvaa. Hatua hiyo iliwafanya mashabiki kuingilia kati kwa kumshangilia na kuimba pamoja naye, hali iliyompa nguvu ya kuendelea na onesho hilo.
Wimbo Somebody’s Son umebeba ujumbe mzito wa mapenzi na matarajio ya maisha ya ndoa, jambo ambalo wengi wanaamini ndilo lililochangia msanii huyo kuguswa kihisia jukwaani.
Ingawa hakutoa maelezo rasmi kuhusu sababu za kuangua kilio hadharani, tukio hilo limeelezwa na mashabiki kama la kugusa na kuonesha upande wa kibinadamu wa msanii huyo. Some Body Son, ni wimbo wa Tiwa savage unaopatikana kwenye EP yake ya Water & Garri alioiachia Mwezi Agosti, mwaka wa 2021.