Msanii wa muziki kutoka Kenya,Toxic Lyrikali, amewagusa wengi mitandaoni baada ya kushare picha ya zamani inayomuonesha akiwa kazini akifanya kazi ya mjengo, miaka kadhaa kabla ya kupata mafanikio kwenye muziki wake.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Toxic Lyrikali ameeleza kuwa picha hiyo ni ukumbusho wa safari yake ya maisha, akisisitiza kuwa mafanikio hayaji kwa njia za mkato bali kwa juhudi, subira na kujituma bila kukata tamaa.
Mashabiki wengi wamempongeza hitmaker huyo wa Back Bencher kwa unyenyekevu na ujasiri wa kuonyesha alikotoka, wakisema ni funzo tosha kwa vijana wanaodharau kazi ndogo au kukata tamaa mapema wanapokosa mafanikio ya haraka.
Kwa mujibu wa mashabiki hao, simulizi ya Toxic Lyrikali inaonyesha wazi kuwa kila kazi halali ina heshima yake, na kwamba mafanikio ni matokeo ya safari ndefu yenye changamoto nyingi.