Msanii nyota kutoka Uganda, Eddy Kenzo, amependekeza wazo la kujengwa kwa makaburi maalum kwa wasanii na wabunifu (creatives) kama njia ya kuhifadhi na kuheshimu urithi wao hata baada ya kifo.
Akizungumza wakati wa ibada ya kuaga mwili wa mama mzazi wa msanii Fik Fameica, Kenzo amesema wasanii wengi hutoa mchango mkubwa katika jamii kupitia sanaa, muziki na ubunifu wao, lakini mara nyingi historia na kazi zao husahaulika wanapofariki.
Hitmaker huyo Sitya Loss, amesema kuwepo kwa makaburi maalum kutasaidia kuhifadhi kumbukumbu zao, kuenzi mchango wao na kuwapa heshima wanayostahili.
Kwa mujibu wa Kenzo, wazo hilo halilengi kuwa sehemu ya mazishi pekee, bali pia kuwa kituo cha kihistoria kitakachoonyesha wasifu, mafanikio na safari za kisanaa za wasanii kutoka fani mbalimbali kama muziki, filamu na sanaa za ubunifu.