Shirika la kukabiliana na utumizi wa dawa za kusisimua misuli michezoni WADA likishirikiana na shirika la kukabiliana na utumizi wa dawa za kusisimua misuli michezoni humu nchini limezindua wakfu wa siku mbili wa kanda ya tano Afrika kuhusu vita dhidi ya utumizi wa dawa zilizoharamishwa michezoni.
Wakfu huo ambao huleta pamoja maafisa wa kuthibiti utumizi wa dawa za kusisimua misuli kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Gambia, Eritrea na Burundi unanuiwa kuwapa mafunzo maafisa hao kuhusu haja ya kuboresha uadilifu katika vita dhidi ya utumizi wa dawa zilizoharamishwa michezoni.
Kenya imepongezwa kwa juhudi zake katika kukabiliana na utumizi wa dawa za kusisimua misuli michezoni huku wito ukitolewa kwa ushirikiano baina ya mashirikisho ya michezo na mashirika ya kukabiliana na utumizi wa dawa haramu michezoni.
Mwezi uliopita, mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za marathoni Ruth Chepng’etich alipigwa marufuku kwa miaka mitatu ilihali aliyekuwa mwanariadha aliyeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 10 Rhonex Kipruto akipigwa marufuku kwa miaka sita mwezi Juni mwaka jana.