Baadhi ya Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wameonyesha wazi kutoridhishwa na msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, wakitishia kususia shoo zake zote zitakazofanyika nchini Kenya baada ya msanii huyo kuwasili nchini humo kwa ziara ya kikazi.
Wengi wao mtandaoni wamesema hawatohudhuria shoo zake, wakimtuhumu kwa kukaa kimya wakati Watanzania walikumbwa na madhila ya kisiasa.
Baadhi wamesisitiza kwamba wasanii wanaochagua kusimama upande wa mamlaka katika kipindi cha misukosuko wanapaswa kuwajibishwa na mashabiki wao.
Hatua hiyo imechochewa na madai kwamba Harmonize aliunga mkono waziwazi serikali ya Rais Samia Suluhu wakati Tanzania ilipokumbwa na mivutano mikubwa ya kisiasa na ripoti za ukandamizaji wa upinzani.