
Mvutano kati ya Megan Thee Stallion na Tory Lanez unaendelea kuchukua sura mpya, huku wakili wa Megan akitoa tamko kali kupitia jarida la XXL baada ya timu ya mawakili wa Tory kuzindua tovuti mpya inayodai kuonyesha ushahidi wa kutetea haki ya msanii huyo.
Tovuti hiyo, iliyoanzishwa na timu ya Tory Lanez, inalenga kushawishi umma kuhusu kutokuwa na hatia kwake katika kesi ya kumpiga risasi Megan Thee Stallion, tukio ambalo lilitokea mwaka 2020 na kumweka Tory kwenye matatizo makubwa ya kisheria.
Katika kujibu hatua hiyo, wakili wa Megan alikemea vikali juhudi za Tory Lanez kujaribu kuandika upya simulizi ya tukio la kumpiga risasi Megan mwaka 2020. Alisema kuwa tovuti hiyo ni jaribio la kuwapotosha mashabiki na kulifanya jambo hili kuwa la burudani badala ya kutafuta haki.
Wakili huyo alisisitiza kuwa Tory tayari alikutwa na hatia kupitia mfumo wa sheria wa Marekani, na kwamba kuendelea kujaribu kujiosha kupitia mitandao na vyombo vya habari ni kudhalilisha wahanga wa ukatili na kuleta mkanganyiko kwa umma.
“Ni aibu kuona mtu anayejaribu kugeuza maumivu ya mtu kuwa kampeni ya mtandaoni. Ukweli ulishasemwa mahakamani, na haki ilitendeka,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa upande wa Tory Lanez, timu yake ya mawakili imeendelea kushikilia kuwa msanii huyo hakutenda kosa lolote, na wanasema tovuti hiyo ni jukwaa la kutoa taarifa walizoita “uhalisia wa tukio.”
Wakati huu, Tory Lanez bado anahudumu kifungo baada ya kupatikana na hatia katika kesi hiyo. Hata hivyo, juhudi za timu yake za kupigania hadhi yake mbele ya macho ya umma zinaendelea kushika kasi, huku wafuasi wa pande zote wakiendelea kupambana mitandaoni kwa maoni na mitazamo tofauti.