
Msanii na Prodyuza wa muziki nchini Kenya Magix Enga amejipata pabaya kwenye mitandao ya kijamii baada ya kudai kuwa yuko tayari kumlipa mchekeshaji Jalang’o shillingi millioni 2 za Kenya kila mwezi ili aachane azma yake ya kujiunga na siasa.
Kauli hiyo ya Magix Enga imeonekana kuwakera watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii ambao wamedai kuwa Prodyuza huyo ana matatizo ya kiakili huku wakimtaka aache suala la kujigamba kuwa ana pesa nyingi wakati anaishi maisha ya uchochole.
Baadhi wameenda mbali zaidi na kuhoji kuwa hatua ya Magix Enga kudai kuwa ni muumini wa dhehebu la illuminati ilikuwa njia ya kutengeneza mazingira ya kuzungumziwa kwenye tasnia ya muziki nchini.
Ikumbukwe juzi kati Magix Enga aliibuka na kudai kuwa alipata mali nyingi alipojiunga na dhehebu la illuminati lakini alipookoka mambo yalianza kumuenda murama hadi akafilisika kiuchumi.