
Wakili wa rapa maarufu Megan Thee Stallion wametoa taarifa rasmi wakikanusha madai ya kambi ya Tory Lanez kuwa kuna ushahidi mpya ambao unaweza kumuondolea hatia kwenye kesi ya kumpiga risasi Megan mwaka 2020.
Katika ripoti yenye kurasa 31 iliyotolewa wiki hii, timu ya sheria ya Megan imeeleza kuwa madai hayo yanayosambazwa ni ya kupotosha na hayana msingi wowote wa kisheria. Wameyataja kama “hadithi za uongo” zinazoenezwa na kile walichokiita “watesi wajinga.”
“Hakuna ushahidi mpya kutoka Ring camera kama inavyodaiwa, na shahidi anayetajwa hajawahi kuwa eneo la tukio, wala kutoa ushahidi wowote hadharani au mahakamani,” alisema wakili Alex Spiro.
Megan Thee Stallion pia aliunga mkono msimamo huo mapema wiki hii, akitoa kauli zinazosisitiza kuwa juhudi za kudhoofisha ukweli ni sehemu ya mateso yanayoendelea dhidi yake kama mhanga wa tukio hilo.
Kesi hiyo iliibua hisia kali za kijamii na mitandaoni, na licha ya hukumu ya mahakama, juhudi za upande wa Tory Lanez kutaka kesi ifunguliwe upya au hukumu ipunguzwe zimeendelea kuchochea mijadala. Hata hivyo, timu ya Megan inasisitiza kuwa hakuna msingi wa kisheria au ushahidi wowote mpya wa kuanzisha mwelekeo tofauti wa kisheria.
Kwa sasa, Tory Lanez anatumikia kifungo gerezani kufuatia hukumu hiyo ya kumpiga risasi Megan, na kesi hiyo inaendelea kuibua mazungumzo kuhusu haki kwa waathirika wa vurugu za silaha, na pia athari za upotoshaji wa umma kwenye kesi nyeti.