
Msanii wa muziki kutoka nchini Uganda, Chris Evans, ametangaza rasmi kuachana na wanawake warembo, akisema hawana nia ya dhati ya kuingia kwenye ndoa.
Evans, ambaye amewahi kuhusishwa kimapenzi na mastaa kama Zanie Brown, Spice Diana, na Lydia Jazmine, amesema kwamba wanawake wengi warembo huwa wanavutiwa na mali na si kujenga familia.
Mwanamuziki huyo anayefahamika kwa kibao chake maarufu “Linda”, amesema kwa sasa moyo wake umeelekezwa kwa wanawake wa muonekano wa wastani, ambao kwa mtazamo wake wana sifa ya unyenyekevu, uaminifu, na nia ya kweli ya kuanzisha ndoa ya kudumu.
“Nimeacha kuwahangaikia wanawake warembo kwa sababu hawana nia ya kweli. Wengi wao wanawinda pesa na hata hawafai kwa ndoa. Nitawachagua wale walio na mwonekano wa wastani kwa sababu huwa ni uaminifu na wako tayari kuanzisha maisha ya ndoa,” alieleza.
Chris Evans amesisitiza kuwa yuko tayari kutulia na mwanamke mmoja na kuanzisha familia yenye misingi imara ya upendo na uaminifu Hatua hii inaonekana kuwa mwanzo mpya kwa msanii huyo mkongwe, ambaye kwa muda mrefu ameonekana kwenye vichwa vya habari kutokana na mahusiano yake ya kimapenzi na mastaa wa tasnia ya burudani nchini Uganda.