
Mwanamuziki wa gengetone Sylvia Ssaru, maarufu kama Ssaru, amefunguka kwa uchungu kuhusu athari za marufuku ya Bodi ya Kudhibiti Kamari nchini Kenya (BCLB) dhidi ya matangazo ya betting kupitia influencers na wasanii.
Akizungumza na SPM Buzz katika mahojiano maalum, Ssaru alisema marufuku hiyo imeathiri moja kwa moja kipato chake na cha wasanii wengine waliokuwa wakitegemea mikataba ya ubalozi kutoka kwa kampuni za kubashiri.
“Ni kama tumetolewa nyama kwa mdomo. Hapa ndo tunatoanga rent, pesa za video. Kuna influencer labda hii ndo deal yake ya kwanza, na sasa they consider themselves jobless,” alisema.
Kauli ya Ssaru imekuja siku chache tu baada ya BCLB kutoa agizo rasmi likipiga marufuku kampuni za kubashiri kutumia influencers, wanablogu, na majukwaa ya mitandao ya kijamii kama sehemu ya mikakati yao ya matangazo.
Katika waraka uliotumwa kwa kampuni mbalimbali, BCLB ilisema kuwa matumizi ya watu maarufu katika kuchochea tabia ya kubashiri ni kinyume na sheria na inahatarisha kizazi cha sasa, hasa vijana.
Hii imeacha pengo kubwa kwa wasanii na maudhui wa dijitali ambao walikuwa wakitegemea kampeni hizo kama chanzo mbadala cha mapato katika tasnia isiyo na uhakika wa kipato wa kila siku.