
Taarifa mpya zimeibuka kuhusu watu waliokuwa wamevaa T-Shirt zenye maandishi “Free Diddy” nje ya mahakama, zikionesha kwamba si wote waliokuja kwa hiari yao. Mwanamke mmoja amefichua kuwa baadhi ya watu waliokuwa wamevalia T-Shirt hizo walikuwa wamelipwa hadi $50 kwa saa ili kushiriki katika kile kinachoonekana kuwa ni kampeni ya kumuunga mkono msanii maarufu, Diddy.
Kwa mujibu wa vyanzo vya burudani nchini Marekani, mwanamke huyo alisema kuwa alikaribishwa kushiriki katika shughuli hiyo lakini alikataa kuvaa T-Shirt hizo licha ya kuahidiwa malipo ya $20 kwa saa mwanzoni, ambayo baadaye yaliripotiwa kuongezeka hadi $50 kwa saa kwa baadhi ya watu.
“Nilijua siwezi kuvaa hiyo T-shirt. Siwezi kusimama nikimuunga mkono mtu ambaye sijui ukweli wake,” alisema mwanamke huyo.
Kampeni ya Free Diddy imezua mjadala mkubwa mtandaoni, huku baadhi ya watu wakihisi kuwa inalenga kuonesha picha ya uungwaji mkono wa umma kwa Diddy wakati mashtaka dhidi yake bado yanaendelea kushughulikiwa mahakamani.
Mpaka sasa, haijafahamika wazi ni nani aliyefadhili kampeni hiyo ya mavazi, lakini madai ya watu kulipwa kushiriki yamezua maswali kuhusu uhalisia na dhamira ya maandamano hayo ya kuunga mkono msanii huyo.