Tech news

WhatsApp Kuanza Kuruhusu Watumiaji Kushiriki Status za Wengine (Repost)

WhatsApp Kuanza Kuruhusu Watumiaji Kushiriki Status za Wengine (Repost)

WhatsApp imeanzisha rasmi majaribio ya kipengele kipya kinachowezesha watumiaji kushiriki (repost) Status za wengine moja kwa moja kwenye Status zao binafsi, bila kulazimika kuomba au kupakua maudhui hayo. Kipengele hiki kwa sasa kinapatikana kwa watumiaji wa toleo la majaribio (beta) kwa Android na iOS, na kinatarajiwa kubadilisha namna watumiaji wanavyoshirikiana kwenye jukwaa hilo.

Kwa kutumia kipengele hiki, mtumiaji atakuwa na uwezo wa kubofya kitufe cha “Repost” chini ya Status ya rafiki, na kuiweka kwenye Status yake papo hapo. Hii ni habari njema kwa wapenzi wa memes, vichekesho, na ujumbe wa haraka, kwani itaondoa hatua za kuomba au kudownload maudhui ya mtu mwingine.

WhatsApp imeweka pia mipangilio ya faragha, ambayo inamruhusu mtumiaji kuchagua nani anaweza kushiriki Status zake.  Hili linahakikisha kuwa faragha inazingatiwa licha ya kipengele hiki kipya kuongeza mwingiliano kati ya watumiaji.

Wachambuzi wa teknolojia wanaamini kipengele hiki kitafanya WhatsApp kuwa karibu zaidi na majukwaa ya kijamii kama Instagram Stories au Facebook Stories, huku ikibaki kuwa salama na ya binafsi zaidi. Kipengele hicho kinatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika usambazaji wa maudhui mtandaoni pindi kitakapoanza kutumika kwa wote.

Kwa sasa, bado hakuna tarehe rasmi ya uzinduzi wa kipengele hiki kwa watumiaji wote duniani, lakini kwa jinsi majaribio yanavyoendelea vizuri, huenda kikaanza kutumika rasmi katika miezi michache ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *