
Mwanamuziki wa Kenya, Willy Paul, ameibua hasira mitandaoni dhidi ya Shirika la Umeme nchini (KPLC) baada ya kudai kuwa vifaa vyake vyote vya studio vimeungua kutokana na hitilafu ya umeme.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Willy Paul alitoa ujumbe mkali kwa KPLC, akisisitiza kuwa wanapaswa kumlipa fidia kwa hasara aliyopata.
“KPLC YOU MUST PAY!! ALL MY STUDIO EQUIPMENTS ARE NO MORE!! MMENICHOMEA KILA KITU KWA STUDIO, NOT JUST ME, THE WHOLE ESTATE HAS LOST VALUABLES!!! KPLC YOU MUST PAY ME!!!!” aliandika kwa ukali.
Msanii huyo, ambaye pia ni mmiliki wa lebo ya muziki, amesema tukio hilo halikumdhuru yeye pekee, bali wakaazi wote wa mtaa anaoshi wamepoteza mali zao kutokana na hitilafu hiyo ya umeme. Ingawa hajatangaza thamani halisi ya vifaa vilivyoharibika, Willy Paul alisisitiza kuwa alikuwa amewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye studio hiyo.
Mashabiki wake wengi wametuma jumbe za kumuunga mkono, huku wengine wakitaka KPLC kuwajibika na kueleza chanzo cha tatizo hilo. Hadi sasa, KPLC haijatoa tamko rasmi kuhusu madai ya msanii huyo.
Wito wake wa kulipwa fidia kutoka KPLC umeibua mjadala mkubwa kuhusu uwajibikaji wa kampuni hiyo katika kusababisha uharibifu wa mali kutokana na hitilafu za umeme, suala ambalo limekuwa likijirudia kwa miaka mingi.