Entertainment

Yammi Afunguka Kwa Mara ya Kwanza Baada ya Kuondoka The African Princess

Yammi Afunguka Kwa Mara ya Kwanza Baada ya Kuondoka The African Princess

Msanii wa muziki wa Bongo, Yammi, ameandika ujumbe mzito wa kihisia katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa leo, ikiwa ni mara ya kwanza kujitokeza hadharani tangu kuachana na lebo ya The African Princess inayoongozwa na Nandy.

Kupitia mtandao wake wa Instagram, Yammi amechapisha ujumbe wa kwanza rasmi tangu aachane na lebo hiyo, akieleza hisia zake za ndani kuhusu safari yake ya muziki, changamoto alizokutana nazo, na matumaini ya mustakabali mpya.

“Leo ni wakati muhimu sana kwangu, safari yangu haijawahi kuwa rahisi. Mipaka yangu imejaribiwa kwa njia ambazo sikuweza hata kufikiria… Kuna muda nilitaka kukata tamaa, lakini kupitia yote nimegundua kuwa lazima nibaki imara na kuendelea kufuata ndoto zangu.” Aliandika

Katika ujumbe huo uliogusa hisia za mashabiki wengi, Yammi alieleza kuwa kila changamoto aliyopitia imemfunza kitu na kumjenga kuwa msanii mwenye maono mapya na nguvu zaidi.

“Kila sehemu na kila jambo limenifundisha vitu. Alhamdulillah… here I come more stronger and determined than ever!” Alimalizia kwa hisia kali.

Mashabiki wake wamemiminika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii wakimpongeza kwa ujasiri na kumtakia mafanikio mema katika hatua yake mpya ya maisha ya muziki. Wengi wamesisitiza kuwa wanamsubiri kwa hamu na shauku kubwa, wakiamini kuwa Yammi bado ana mengi ya kuonyesha duniani.

Yammi, ambaye alifahamika kupitia vibao kama “Namchukia” na “Tunayoyaweza”, alikuwa mmoja wa wasanii waliokuwa wakikuzwa chini ya lebo ya The African Princess, inayomilikiwa na Nandy. Tangu kuingia kwake kwenye tasnia ya muziki, ameonyesha uwezo mkubwa wa sauti, hisia, na utunzi wa hali ya juu.

Uamuzi wake wa kuachana na lebo hiyo bado haujaelezwa kwa kina, lakini ujumbe wake wa kihisia unaashiria mwanzo mpya na ari ya kuendelea kupambana ili kufanikisha malengo yake ya kisanii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *