
Rapa mwenye utata na mabadiliko ya ghafla, Kanye West, anayejulikana pia kama Ye, ameandika ujumbe mzito wa toba kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), akiomba msamaha kwa Mungu kwa maumivu aliyowahi kusababisha, huku akitangaza kuwa amewasamehe wote waliomuumiza.
Katika ujumbe huo uliojaa hisia, Ye alisema ameacha kabisa chuki aliyokuwa nayo dhidi ya Wayahudi, na sasa anawapenda watu wote bila ubaguzi.
“Nimeomba msamaha kwa Mungu. Nimewasamehe waliotenda mabaya dhidi yangu, na sasa nawafurahia wanadamu wote,” aliandika rapa huyo.
Ye pia aligusia mawasiliano ya karibu na watoto wake, akieleza kuwa waliwasiliana naye kwa FaceTime tu,kio lililomgusa sana na kuonekana kuwa na nafasi maalum katika mabadiliko yake ya kiroho na kibinadamu.
Ujumbe wake umezua maoni mseto miongoni mwa mashabiki. Wengine wamepokea hatua hiyo kama mwanzo mpya kwa msanii huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa matamshi yenye utata na msimamo mkali kuhusu masuala ya kidini, kisiasa na kijamii.
Tangazo hili linakuja baada ya kipindi kirefu cha shutuma nzito kutokana na matamshi yake yaliyotafsiriwa kama chuki dhidi ya Wayahudi, na hata kusababisha kupoteza mikataba mikubwa ya kibiashara. Toba yake sasa imechukuliwa kama jaribio la kurejesha uhusiano na jamii na pia kurekebisha taswira yake kwa umma.
Hadi sasa, ujumbe huo tayari umepata maelfu ya likes na maoni, wengi wakisubiri kuona kama mabadiliko haya ni ya kudumu au ni sehemu nyingine ya mzunguko wa tabia za Ye ambazo mara nyingi husababisha taharuki mitandaoni.