
Jukwaa kubwa la kushiriki video duniani,YouTube, limetangaza kuwa litaondoa rasmi ukurasa wake wa Trending kuanzia Julai 21. Hatua hii ni sehemu ya mabadiliko yanayolenga kuboresha namna watumiaji wanavyogundua maudhui mapya na yanayovuma.
Kwa muda mrefu, sehemu ya Trending imekuwa ikionesha video maarufu zinazopata watazamaji wengi kwa kipindi kifupi. Hata hivyo, YouTube imeamua kuachana na ukurasa huo kwa kuwa haukuwa unawakilisha ipasavyo utofauti wa maudhui au maslahi binafsi ya watumiaji wake.
Badala yake, YouTube itazingatia zaidi matumizi ya ukurasa wa Explore (Gundua), ambao tayari unawasaidia watumiaji kugundua video kupitia mada mbalimbali kama vile muziki, michezo, teknolojia, mitindo na zaidi. Ukurasa huu pia unaonesha video zinazovuma kwa upana zaidi na kwa kuzingatia eneo la mtumiaji.
Mabadiliko haya yanatarajiwa kuwasaidia watumiaji kupata maudhui yanayolingana zaidi na mapendeleo yao binafsi, badala ya orodha moja ya video zinazotazamwa zaidi kwa ujumla. Kwa wabunifu wa maudhui, hatua hii inafungua fursa ya kufikiwa na watazamaji wapya kupitia mapendekezo ya mfumo wa YouTube.
Mabadiliko haya yataanza kutekelezwa rasmi tarehe 21 Julai, ambapo sehemu ya Trending itaondolewa kabisa kutoka kwenye menyu ya YouTube na nafasi yake kuchukuliwa na vipengele vilivyoboreshwa vya Explore.