YouTube imetangaza kusitisha rasmi kushirikisha takwimu zake za muziki na jarida maarufu la chati za muziki, Billboard. Hatua hii itasababisha Billboard kutozitumia tena data za YouTube katika kuandaa chati zake za muziki.
Kwa mujibu wa YouTube, uamuzi huo umetokana na kutokubaliana kati ya pande hizo mbili kuhusu namna takwimu za streams zinavyotumika kupima umaarufu wa nyimbo.
YouTube imesema kuwa matumizi ya jukwaa lake ni tofauti na huduma za kawaida za kusikiliza muziki, ikieleza kuwa streams nyingi hutokana na autoplay, kusikiliza kwa nyuma, pamoja na aina mbalimbali za video, hivyo si kila stream ni chaguo la moja kwa moja la msikilizaji.
Kutokana na hali hiyo, YouTube inaamini kuwa kuzihesabu streams zake sawa na zile za apps za muziki ni kupotosha uhalisia wa umaarufu wa nyimbo.
Aidha, YouTube imetangaza kuwa itaweka kipaumbele kwenye chati zake binafsi, yaani YouTube Music Charts, kama kipimo rasmi cha kupima umaarufu wa muziki ndani ya jukwaa hilo.
Mabadiliko haya yanatarajiwa kuanza rasmi kuanzia tarehe 16 Januari 2026, na tayari yamezua mjadala mpana ndani ya tasnia ya muziki kuhusu namna mafanikio ya nyimbo yanavyopimwa duniani.