
Msanii wa dancehall kutoka Uganda, Ziza Bafana, amenyoosha maelezo kuhusu madai yaliyosambaa mtandaoni kwamba alifukuzwa nchini Uholanzi siku chache zilizopita.
Akizungumza na wanahabari, Bafana ameeleza kuwa alikuwa amepangiwa maonyesho mawili mjini Amsterdam na Ujerumani. Hata hivyo, alipowasili Amsterdam aliombwa kuonesha kibali cha kazi, ambacho kwa bahati mbaya hakuwa nacho, na hivyo akazuiliwa kuendelea na ratiba yake.
Mkali huyo wa Speed Controlle amesisitiza kuwa hakufukuzwa kama baadhi ya wakosoaji walivyodai kwenye mitandao ya kijamii. Badala yake, amefafanua kuwa tatizo lilitokana na ukosefu wa vibali sahihi vya kazi.
Bafana ameilaumu mamlaka za usafiri za Uganda kwa kusababisha kuvurugika kwa shoo zake, akisema uzembe wa maandalizi ya nyaraka muhimu ndio uliosababisha kufutwa kwa maonesho yake yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa kimataifa.
Kwa sasa, msanii huyo ameahidi kuchukua hatua kuhakikisha taratibu zote za kisheria zinafuatwa ili kuepusha changamoto kama hizo siku za usoni, huku akiomba mashabiki wake waendelee kumpa sapoti licha ya changamoto alizopitia.