WhatsApp imeanza majaribio ya kubadilisha sehemu ya “About Status” kwa kuifanya ifanye kazi kama sehemu ya Instagram Notes. Mabadiliko haya yanawalenga watumiaji wanaotaka kuandika ujumbe mfupi unaoonekana kwa muda maalum bila kutuma ujumbe moja kwa moja au kuweka status ya kawaida.
Kupitia kipengele hiki kipya, mtumiaji ataweza kuchagua kuandika ujumbe mfupi ambao utaonekana kwa muda maalum kama saa 1, masaa 8, siku 2, au hata wiki moja, kutegemea na chaguo lake. Ujumbe huu utaonekana pembeni ya picha ya mtumiaji (profile picture) na utaweza kuonekana kwa urahisi na watu ambao wanaendelea kuchati naye, bila kulazimika kufungua taarifa ya mtumiaji husika.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka WhatsApp, lengo la sehemu hii mpya ni kurahisisha mawasiliano ya haraka kati ya watumiaji na marafiki wao. Ni njia mbadala ya kuonyesha hali yako au ujumbe muhimu kwa muda mfupi, tofauti na status ya kawaida inayodumu kwa saa 24.
Kwa sasa, kipengele hiki kipo kwenye hatua ya majaribio kwa baadhi ya watumiaji, na kinaweza kuzinduliwa kwa watumiaji wote katika toleo lijalo la programu.
Mabadiliko haya yanaonyesha juhudi za WhatsApp kuendelea kuimarisha mawasiliano ya kijamii kwa kutumia vipengele rahisi lakini vyenye athari katika matumizi ya kila siku.