Briefs

Raila Odinga afariki dunia nchini India

Raila Odinga afariki dunia nchini India

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 nchini India, vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti.

Kwa mujibu wa taarifa, Raila aliaga dunia kutokana na mshtuko wa moyo (cardiac arrest) alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Kochi, nchini India.

Vyanzo vya karibu na familia vinaeleza kuwa Odinga alikuwa amesafiri India wiki moja iliyopita kwa uchunguzi wa kiafya na matibabu ya ufuatiliaji. Madaktari walijaribu kumhudumia kwa muda mrefu, lakini jitihada zao hazikuzaa matunda.

Odinga, ambaye amekuwa mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa katika historia ya Kenya, alihudumu kama Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2008 hadi 2013 katika serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki. Aidha, aliwahi kuwa Mbunge wa Lang’ata, Waziri wa Nishati, na baadaye Waziri wa Barabara kabla ya kuunda chama cha ODM kilichompa umaarufu mkubwa.

Raila pia alikuwa kiongozi wa upinzani kwa miongo kadhaa, akigombea urais mara kadhaa bila kufanikiwa, huku akiendelea kuwa sauti kuu ya mageuzi ya kisiasa na utetezi wa demokrasia nchini Kenya.

Kifo chake kimetokea wakati ambapo alikuwa akijihusisha na shughuli mbalimbali za kisiasa na maandalizi ya mageuzi ya Afrika kupitia Umoja wa Afrika (AU).

Wakenya wengi wameelezea huzuni na mshtuko mkubwa kufuatia taarifa hizo, huku mitandao ya kijamii ikifurika jumbe za rambirambi, baadhi wakimtaja kama “Baba wa taifa la pili” kwa mchango wake mkubwa katika harakati za kidemokrasia na kupinga ukandamizaji wa haki za wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *