Mwanamitandao Diana Marua ameonyesha kuguswa sana na mapenzi na heshima anayopokea kutoka kwa mtoto wake wa kambo Morgan Bahati, akieleza kuwa mara nyingi mtoto huyo humfanyia mambo ya kumfariji na kumfanya ajisikie kuthaminiwa kama malkia.
Kupitia ujumbe mrefu aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Diana amesema kuwa Morgan huwa anaonyesha upendo mkubwa kwa familia na mara nyingi hujitolea kuhakikisha kila mtu anajisikia vizuri nyumbani.
Diana, amefichua kuwa wakati mwingine Morgan humfanyia masaji ya miguu wanapokuwa pamoja nyumbani, jambo ambalo huwapa nafasi ya kuzungumza, kubadilishana mawazo na kuimarisha zaidi uhusiano wao wa mama na mwana.
Mwanamama huyo, amesema nyakati kama hizo humkumbusha safari ndefu waliyopitia pamoja tangu alipomlea Morgan, akibainisha kuwa anaona fahari kuona namna mtazamo wa maisha wa kijana huyo umebadilika na kukua kwa kiasi kikubwa.
Aidha ameeleza furaha yake baada ya Morgan kujiunga na mojawapo ya shule bora za kitaifa nchini Kenya, Lenana School. Tukio hilo lilimfanya kuwa na hisia kali za furaha na shukrani kwa mafanikio ya mtoto huyo.
Diana amesisitiza kuwa anaamini familia yao imebarikiwa sana, huku akimshukuru Morgan kwa kumpa nafasi ya kuitwa mama yake na kuahidi kuendelea kumuombea baraka na mafanikio katika maisha yake ya baadaye.