
Baada ya wiki ya taharuki na mivutano ya hadharani iliyopelekea kurushiana lawama mitandaoni, mchekeshaji Mulamwah na aliyekuwa mpenzi wake Ruth K wameamua kufunga ukurasa wa mgogoro huo kwa kuomba msamaha kwa mashabiki wao, kila mmoja akielezea majuto yake kwa yaliyojiri.
Kupitia ujumbe mrefu aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mulamwah alielezea kwa kina maumivu na majuto aliyobeba kufuatia kile alichokieleza kama msururu wa maamuzi yasiyo ya busara aliyoyafanya akiwa chini ya hisia kali. Alisema kuwa amefanya tafakari ya kina na ametambua kuwa matendo yake yalikuwa ya kuumiza na ya kutozingatia hisia za wengine.
“Poleni sana kwa mashabiki wangu wote. Najua nimewaangusha kwa njia nyingi. Nilikuwa nimesukumwa na hisia na hali mbalimbali, lakini hiyo haifai kuwa sababu ya mimi kufanya baadhi ya mambo niliyofanya. Nimejifunza, nimejirekebisha, na nipo tayari kuanza upya,” alisema Mulamwah katika ujumbe wake wa maombi ya msamaha.
Mulamwah alihitimisha kwa kueleza kuwa ni wakati wa kutuliza hali, kusonga mbele na kuweka nguvu katika kazi na malezi, huku akimwomba Mungu kuwaongoza katika maamuzi ya baadaye.
Kwa upande wake, Ruth K naye hakusita kuonesha unyenyekevu wake kwa mashabiki na familia yake. Katika chapisho lake, aliomba msamaha kwa wale wote waliokwazwa na matendo au kauli zake, na akaahidi kuanza ukurasa mpya wa maisha.
“Ninachukua jukumu kamili kwa sehemu yangu ya makosa. Nilikuwa nikipitia wakati mgumu kihisia na kwa kweli mambo mengi yalinitesa. Si kila nilichofanya kilikuwa sahihi, lakini naomba mnisamehe. Nitakuwa bora – kwa ajili yangu, kwa ajili ya mtoto wangu, na kwa ajili yenu,” alisema.
Aliongeza kuwa kama mama wa mtoto mmoja, anapitia changamoto nyingi huku akijitahidi kudumisha utu na utulivu. Ruth aliomba msamaha kwa wote walioumizwa au kuvunjwa moyo na matendo yake, na kueleza kuwa huu ni mwanzo mpya wa maisha yenye maadili na nidhamu.
Kuomba radhi kwao kumepokelewa kwa hisia mseto na wafuasi wao, wengi wakikiri kuwa ni hatua muhimu ya ukomavu na uwajibikaji. Wengi wana matumaini kuwa huu ni mwanzo wa ukurasa mpya katika maisha yao binafsi na ya kitaaluma.