
Mchekeshaji maarufu DJ Shiti amesifu juhudi za kundi la Matata, akieleza kuwa wameinua hadhi ya muziki wa Gengetone na kuupeleka kwenye kiwango kipya cha ubunifu na ubora.
Akizungumza katika kipindi cha Mic Cheque Podcast, DJ Shiti ameeleza kuwa amevutiwa na namna kundi hilo limekuwa likiendesha matamasha yao kwa weledi na ubunifu wa hali ya juu. Ameongeza kuwa muziki wa Gengetone umepata hadhi mpya kutokana na juhudi za Matata.
Kulingana naye, kundi hilo limeweza kuboresha mtindo wa Gengetone na kuupanga upya kwa njia ya kitaalamu, hatua ambayo imefanya mashabiki wengi kuupokea kwa mtazamo chanya zaidi tofauti na awali ambapo baadhi waliona Gengetone ni muziki unaohusiana na maisha ya uhuni na anasa.
Matata kwa sasa wanatambulika kama moja ya vikundi vinavyoibua ari mpya katika muziki wa vijana nchini, wakichanganya midundo ya Gengetone na ladha za kimataifa ili kufikia hadhira pana zaidi.