
Msanii aliyegeukia siasa, Bahati, amemtolea uvivu bila huruma mtangazaji wa Radio 47, Fred Arocho, kufuatia kauli za kumkosoa kwa kuchelewa kutimiza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni moja kwa Harambee Stars.
Kupitia Instagram, Bahati amejigamba kuwa ana uwezo mkubwa kifedha na hata akitaka anaweza kumpigia mmiliki wa Radio 47 sasa hivi na kununua kituo hicho. Amesema pia yuko tayari kumweka mke wake, Diana Marua, kama boss wa kituo hicho cha redio ambacho Arocho hufanyia kazi, akisisitiza kwamba pesa kwake si tatizo.
Haikuishia hapo amejinasibu kuhusu utajiri wake, kwa kusema kwamba kwa wiki moja hutumia shilingi milioni tatu, na hata baada ya mwaka mmoja bila kutoa wimbo mpya bado anaendelea kustawi kifedha.
Hitmaker huyo wa Pete yangu, amefafanua kuwa kuchelewa kutoa mchango wake hakumaanishi hana nia ya kusaidia. Ameeleza kwamba alikuwa amejiandaa kwa muda wa wiki nzima kuandaa sherehe kubwa ya kuzaliwa kwa mtoto wake, hafla ambayo hakutaka kuiahirisha kwa ajili ya kutoa mchango huo.
Hata hivyo, Bahati amelalamika kwamba hata pale alipokuwa tayari kuwasilisha mchango wake kwa timu ya taifa, hakukuwa na mtu aliyejitokeza rasmi kupokea, akimlaumu kiungo wa zamani wa Harambee Stars McDonald Mariga kwa kutopokea simu zake.
Kauli ya Bahati inakuja wiki moja baada ya, Arocho kueleza kutoridhishwa na ahadi ya msanii huyo kwa timu ya taifa akisema kwamba mashabiki na wachezaji wa Harambee Stars walikuwa wakisubiri kwa matumaini makubwa msaada huo, na kuchelewa kwake kumeonekana kama njia ya kujitafutia kiki.