Google inapanga kuanzisha mabadiliko makubwa kwenye huduma yake ya barua pepe ya Gmail kuanzia mwaka 2026, ambapo watumiaji wataruhusiwa kubadilisha username za barua pepe zao bila kufungua akaunti mpya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mtumiaji ataweza kurekebisha anwani yake ya barua pepe kwa urahisi. Kwa mfano, mtu mwenye barua pepe urbanspice254@gmail.com ataweza kuibadilisha na kuwa urbanspice@gmail.com au jina jingine analolipendelea, endapo litakuwa halijatumika.
Hatua hii inalenga kuwasaidia watumiaji wanaotamani kuwa na barua pepe zilizo safi zaidi, hasa kuondoa namba, tarehe au majina yasiyo rasmi waliyotumia zamani.
Google imesisitiza kuwa mabadiliko hayo hayatathiri taarifa za mtumiaji, kwani barua pepe zote zilizopo kwenye inbox, sent na data nyingine zitaendelea kubaki salama. Aidha, anwani ya zamani itaendelea kupokea barua pepe, ambazo zitakuwa zikielekezwa moja kwa moja kwenye anwani mpya.