Msanii wa Bongo Fleva Harmonize amemvisha rasmi mwanamama Kajala Masanja pete ya uchumba katika hafla ya faragha iliyofanyika leo ndani ya boti, hatua iliyoashiria kurejea kwao rasmi katika mahusiano.
Hafla hiyo maalum iliandaliwa kusherehekea mapenzi yao, ikihudhuriwa na marafiki wa karibu pekee. Wawili hao wameonekana wenye furaha na ukaribu mkubwa, hali iliyovutia mashabiki wao waliopata taswira za tukio hilo kupitia mitandao ya kijamii.
Mpambe wa burudani Mwijaku, aliyekuwepo kwenye tukio la uchumba, amesema Harmonize amemheshimisha kwa kuhalalisha mahusiano yake na Kajala mbele ya zaidi ya watu 100 waliokuwapo, huku akiwatakia wawili hao baraka katika safari yao ya mapenzi.
Hatua hii imekuja siku chache baada ya Harmonize kuthibitisha mahusiano yao juzi kati huko Zanzibar, ambako walizua gumzo kubwa baada ya kuonekana wakibadilishana mabusu hadharani mbele ya mashabiki.