
Mwanamitindo na mwanaharakati Amber Rose ameeleza hadharani sababu za kumtetea msanii Tory Lanez katika kesi ya kumpiga risasi Megan Thee Stallion mwaka 2020. Akizungumza kwenye mahojiano ya moja kwa moja katika kipindi cha Chris Cuomo kinachorushwa kupitia NewsNation, Rose alisema anaamini Lanez hana hatia na anastahili kusamehewa na Gavana wa California, Gavin Newsom.
Katika mazungumzo hayo, Amber Rose alisisitiza kuwa ushahidi uliopo hauonyeshi moja kwa moja kuwa Tory ndiye alifyatua risasi. Alisema Lanez ameshathibitishwa kuwa hana uhusiano wa moja kwa moja na silaha iliyotumika, jambo linaloonyesha kuwa alipaswa kuachiliwa huru.
Chris Cuomo, hata hivyo, aliibua hoja kuwa sampuli za DNA zilionyesha kuwa silaha hiyo ilikuwa inaweza kuguswa na watu wanne tofauti, lakini pia akaongeza kuwa Lanez alituma ujumbe wa kuomba msamaha baada ya tukio hilo, huku Megan Thee Stallion na rafiki yake Kelsey, waliokuwepo usiku huo, wakimtaja Lanez kama mtu aliyefyatua risasi.
Amber Rose alijibu kwa kusema kuwa amesikia simulizi nzima kutoka kwa Tory Lanez mwenyewe, ambaye alimpigia simu moja kwa moja kutoka gerezani na kumueleza kile kilichotokea usiku huo.
Kauli hii ya Amber Rose imezua maoni mseto mitandaoni, huku baadhi wakimtetea kwa kuonyesha huruma na kutaka haki ya kweli itendeke, huku wengine wakimtuhumu kwa kupuuza ushahidi wa upande wa Megan Thee Stallion.
Haya yanakuja siku chache baada ya Amber Rose kuchapisha kipande cha video kinachomuonyesha Mwakilishi wa Bunge la Marekani, Anna Paulina, akimwambia Cuomo kuwa Tory Lanez hana hatia na kwamba kesi hiyo ililetwa kwake na Amber Rose mwenyewe.