
Mtangazaji na mwanahabari maarufu Andrew Kibe amevunja ukimya na kujibu madai yanayomhusisha na Director Trevor, akisema kuwa taarifa kwamba aliwahi kumwomba msaada si za kweli. Kibe anasema kwa uwazi kuwa ni Trevor ndiye aliyekuwa akimtafuta mara kwa mara kupitia ujumbe wa moja kwa moja (DMs) alipokuwa Marekani, kipindi ambacho Trevor alikuwa bado kwenye uhusiano na Mungai Eve.
Kwa mujibu wa Kibe, Trevor alikuwa akimuomba msaada wa kumsadia kufungua upya ukurasa wake wa Facebook, na sasa anamtaka aweke wazi jumbe hizo kwa umma ili ukweli ujulikane.
“Ningependa Trevor aonyeshe jumbe alizoniandikia wakati akinitafuta msaada. Aache kupotosha watu,” alisema Kibe kwa msisitizo.
Mbali na hayo, Kibe amemkosoa Trevor kwa kile alichokitaja kama tabia ya kutafuta umaarufu wa haraka (clout) kwa kutumia majina ya watu maarufu. Amemshauri aweke kando drama zisizo na msingi na ajikite kwenye kazi halali zitakazompa heshima na mafanikio ya kweli. Pia, amemwonya kuhusu kuweka mahusiano kwenye mitandao, akisema hatua hiyo huweza kuishia kwa fedheha kama ilivyotokea kwa msanii Mulamwah.
Kauli hiyo ya Kibe imejibu shutuma zilizotolewa awali na Trevor, aliyedai kuwa Kibe alimdhalilisha kwa kumuita “mwanaume asiyekuwa na msimamo na aliyekaliwa na mwanamke”, kufuatia kuvunjika kwa mahusiano yake na Mungai Eve. Trevor alisema maneno hayo yalimuumiza kihisia na kudhoofisha heshima yake binafsi.
Hata hivyo, Trevor amesema amepitia mengi, lakini kwa sasa amepona kihisia, amejijenga upya, na anaendelea kujiimarisha kimaisha na kitaaluma. Amedai kuwa licha ya changamoto alizopitia, ameibuka kuwa mtu mpya mwenye maono mapya.
Mvutano huu kati ya wawili hao maarufu umechochea mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku mashabiki wakiwa wamegawanyika kati ya wanaomuunga mkono Kibe na wale wanaompigia debe Trevor. Wapo wanaosema drama hii ni ya kutafuta kiki, huku wengine wakitaka wahusika waache tofauti zao na wajikite kwenye kazi.