
Kampuni ya Apple imetangaza kuwa mfumo wao mpya wa uendeshaji, iOS 19, utakuja na kipengele cha kipekee cha kudhibiti matumizi ya betri kwa kutumia akili bandia (AI). Teknolojia hii mpya inalenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati kwenye simu kwa kuzingatia tabia ya mtumiaji. Kwa mfano, iOS 19 itaweza kutambua ni programu zipi unazotumia mara kwa mara na kwa muda gani, kisha itadhibiti matumizi ya umeme kulingana na hilo.
Kipengele hiki kitaendesha kazi zake moja kwa moja bila kuhitaji usaidizi wa mtumiaji, na kitajifunza tabia zako kwa muda ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Hii ina maana kuwa simu yako itaweza kuhifadhi chaji kwa muda mrefu zaidi, bila kuathiri utendakazi wa programu muhimu unazozitumia kila siku.
Mbali na hayo, Apple pia itaongeza kiashiria kipya kwenye skrini ya kufunga (lock screen), ambacho kitaonyesha makadirio ya muda unaohitajika kuchaji simu yako hadi kufikia asilimia 100. Kiashiria hicho kitaongozwa na hali ya afya ya betri yako, matumizi yako ya simu, pamoja na programu zinazoendelea kufanya kazi. Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni ya simu kutumia AI kwa njia ya moja kwa moja katika kuboresha maisha ya betri kwa kiwango hiki.apple