Watangazaji wa Radio 47 Wamchana Bahati kwa Kauli ya Kununua Kituo Chao

Watangazaji wa Radio 47 Wamchana Bahati kwa Kauli ya Kununua Kituo Chao

Watangazaji maarufu wa Radio 47, Alex Mwakideu na Emmanuel Mwashumbe, wamemtolea uvivu msanii Bahati kufuatia kauli yake kwamba angeweza kununua kituo cha Radio 47 pamoja na TV47 na kisha kumpa mke wake, Diana Marua, nafasi ya ubosi ili amsimamie mtangazaji Fred Arocho. Katika kipindi cha asubuhi cha kituo hicho leo, Mwakideu na Mwashumbe walionekana kukerwa na matamshi ya Bahati, wakimtaka aache kujisifu na kudanganya mashabiki wake kuhusu uwezo wake kifedha. Walisema kuwa madai ya Bahati ni ya uongo kwani hana uwezo wa kununua kampuni ya Cape Media, wamiliki wa Radio 47 na TV47. Kauli ya Bahati ilikuja baada ya Arocho kumshinikiza kutimiza ahadi yake ya shilingi milioni moja aliyoitoa kwa Harambee Stars. Msanii huyo alijibu kwa kejeli akidai kwamba akikasirika anaweza hata kununua kituo hicho na kumfanya Diana Marua kuwa bosi wa Arocho. Hata hivyo, watangazaji hao walisema maneno ya Bahati hayana msingi, wakimtupia vijembe kwamba kama kweli ana uwezo huo, basi aanze kwanza kwa kumudu mishahara yao. “Wee huna pesa! Usiwadanganye watu,” waliongeza kwa dhihaka, wakimshauri aendelee na kazi yake ya muziki badala ya kuingilia masuala ya vyombo vya habari. Hali hii imezua gumzo mitandaoni, huku mashabiki wakigawanyika kati ya wanaomuunga mkono Bahati na wale wanaosema amejipata pabaya baada ya kuwakera watangazaji wenye ushawishi mkubwa.

Read More
 Bahati Aomba Ulinzi Baada ya Majambazi Kuvamia Nyumba Yake

Bahati Aomba Ulinzi Baada ya Majambazi Kuvamia Nyumba Yake

Msanii wa muziki, Bahati, ameibua taharuki baada ya kudai kwamba nyumba yake ilivamiwa na majambazi waliokuwa na silaha mapema alfajiri. Kwa mujibu wa Bahati, tukio hilo lilitokea kati ya saa 10:27 alfajiri na saa 11:30 asubuhi, na kuacha familia yake katika hali ya hofu. Ameeleza kuwa uvamizi huo umetokea siku chache tu baada yake na mkewe, Diana Marua, kuonyesha hadharani mafungu ya pesa taslimu yenye thamani ya mamilioni wakiwa ndani ya nyumba yao, jambo ambalo huenda liliwavutia wahalifu. Kupitia mitandao ya kijamii, Bahati ameeleza kuwa ana hofu kubwa kuhusu usalama wa familia yake na sasa ameomba moja kwa moja Inspekta Jenerali wa Polisi kuingilia kati na kutoa ulinzi wa haraka. Tukio hilo limekuja saa chache tu baada ya Bahati kuwatolea uvivu wakosoaji wake waliodai ameshindwa kutimiza ahadi ya kutoa shilingi milioni moja. Akizungumza jana akiwa na msanii DK kwenye Beat, Bahati alionekana akibeba shilingi milioni tatu taslimu, akisisitiza kwamba ana utajiri mkubwa na hawezi kushindwa na jambo dogo kama hilo. Hata hivyo, hatua yake ya kuonyesha mafungu ya pesa taslimu nyumbani huenda ikawa imewachochea wahalifu waliovamia makazi yake.. Tukio hili limezua gumzo mitandaoni, ambapo baadhi ya mashabiki wamemlaumu kwa kuonyesha utajiri wake hadharani, huku wengine wakimuonea huruma na kushinikiza mamlaka kuchukua hatua za haraka.

Read More
 WCB Yakanusha Vikali Taarifa za Zuchu Kukataa Kushirikiana na Wasanii wa Kenya

WCB Yakanusha Vikali Taarifa za Zuchu Kukataa Kushirikiana na Wasanii wa Kenya

Uongozi wa lebo ya muziki ya WCB Wasafi umejitokeza kukanusha taarifa zinazozagaa mitandaoni zikidai kuwa msanii wao, Zuchu, amekataa kushirikiana na wasanii wa Kenya kwa madai kwamba baadhi ya Wakenya walimtukana Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye mitandao ya kijamii. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, WCB imesisitiza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote na ni njama za kuzua mtafaruku kati ya mashabiki wa pande mbili. Uongozi huo umesema kuwa Zuchu hana uhusiano wowote na kauli inayodaiwa kunukuliwa kwenye moja ya blogu nchini Kenya, na kwamba msanii huyo ameendelea kuwa na uhusiano mzuri wa kikazi na mashabiki wake kote Afrika Mashariki. Taarifa hizo za WCB zimekuja muda mfupi baada ya uvumi huo kushika kasi mtandaoni, hasa baada ya kufufuliwa kwa nakala ya blogu iliyodai kuwa Zuchu alinukuliwa akisema hatafanya kazi na wasanii kutoka Kenya. Zuchu kwa sasa yupo nchini Kenya ambapo anatarajiwa kutumbuiza kesho kwenye fainali za CHAN zitakazofanyika kesho kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani. Atashiriki jukwaa moja na Savara wa Sauti Sol kutoka Kenya pamoja na Eddy Kenzo wa Uganda.

Read More
 ByteDance Yaipita Meta kwa Mapato kwa Mara ya Kwanza

ByteDance Yaipita Meta kwa Mapato kwa Mara ya Kwanza

Kampuni ya ByteDance, mmiliki wa mtandao maarufu wa TikTok, imefikia hatua kubwa baada ya kwa mara ya kwanza kuipita kampuni ya Meta katika suala la mapato, tukio ambalo linashuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya mitandao ya kijamii duniani. Kwa ripoti ya robo ya pili ya mwaka 2025 (Q2 2025), ByteDance imepata mapato ya dola bilioni 48, sawa na takriban shilingi trilioni 6.2 za Kenya, ikilinganishwa na Meta iliyopata mapato ya dola bilioni 47.5, yaani takriban shilingi trilioni 6.14 za Kenya. Hii ni mara ya kwanza ByteDance kuipita Meta kwa mapato na kuwa kampuni ya kwanza inayomiliki mitandao ya kijamii kuifanya hivyo. Ukuaji huu mkubwa wa mapato umechangiwa sana na umaarufu mkubwa wa TikTok duniani, hasa miongoni mwa vijana, ambao wamekuwa wateja wakubwa wa jukwaa hilo. Kuongezeka kwa watumiaji na uwekezaji mkubwa wa matangazo kumeongeza mapato ya ByteDance kwa kiwango kikubwa, na hivyo kuifanya kampuni hiyo kuweza kushindana moja kwa moja na Meta, ambayo inamiliki mitandao maarufu kama Facebook, Instagram, na WhatsApp. Meta kwa upande wake imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kupungua kwa mapato ya matangazo na ushindani mkali kutoka kwa majukwaa mapya kama TikTok. Hali hii imesababisha mabadiliko katika mikakati ya biashara ya Meta ili kuweza kudumisha ushindani wake.

Read More
 NOCK Yasisitiza Usawa kwa Wanariadha Wote kuelekea Olimpiki

NOCK Yasisitiza Usawa kwa Wanariadha Wote kuelekea Olimpiki

Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki nchini Kenya (NOCK) imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha kila mwanariadha nchini anapewa nafasi sawa ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa, ikiwemo Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya Dakar na Olimpiki ya Los Angeles mwaka 2028. Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa NOCK, Shadrack Maluki, wakati wa mkutano wake na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Michezo, Dan Wanyama. Maluki alieleza kuwa NOCK inalenga kuhakikisha hakuna talanta inayopuuzwa, huku ikiweka mikakati madhubuti ya kutambua, kukuza na kuendeleza wanamichezo kutoka kila kona ya nchi. Kwa upande wake, Dan Wanyama aliahidi kuwa Bunge litaendelea kushirikiana kwa karibu na NOCK ili kuboresha mazingira ya michezo nchini. Alisisitiza umuhimu wa kuwa na sera imara, miundombinu bora, pamoja na uwekezaji wa kutosha katika maendeleo ya michezo, ili kuhakikisha Kenya inaendelea kung’ara katika majukwaa ya kimataifa. Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya wadau wa michezo na serikali kuhakikisha kuwa Kenya inatuma timu zenye ushindani mkubwa kwenye mashindano yajayo ya kimataifa, huku vijana wakipewa nafasi ya kujifunza, kushindana, na kuiwakilisha nchi kwa fahari.

Read More
 Bobi Wine Adai Serikali Inatumia Mabwenyenye Kudhibiti Muziki Uganda

Bobi Wine Adai Serikali Inatumia Mabwenyenye Kudhibiti Muziki Uganda

Msanii aliyegeukia siasa, Bobi Wine, ameendelea kutoa maoni yake kuhusu changamoto zinazokumba sekta ya muziki nchini Uganda. Wine, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa katika muziki kwa zaidi ya miaka kumi na tano kabla ya kuingia kwenye siasa na hata kuwania urais, anasema sekta hiyo sasa inadhibitiwa na makundi yenye ushawishi makubwa yanayofanya kazi kwa niaba ya serikali. Kwa mujibu wake, serikali inalenga kuhakikisha hakuna msanii mwingine anayeweza kufikia kiwango cha ushawishi alichopata kupitia muziki wake, hivyo kuzuia sanaa kutumika kama chombo cha kuibua sauti za upinzani. Anaeleza kuwa muziki nchini humo umekuwa chombo kinachodhibitiwa kwa karibu, ambapo kila kinachozalishwa studio kinasimamiwa kwa lengo la kudhibiti ujumbe unaofika kwa wananchi. Licha ya kuingia kwenye siasa, Bobi Wine ameendelea kurekodi na kutoa nyimbo, akisisitiza kuwa wasanii wana jukumu la kueleza hali halisi ya jamii. Anawahimiza wanamuziki wenzake kutumia sanaa si tu kwa burudani, bali pia kama jukwaa la kuzungumzia changamoto za kijamii na dhuluma zinazowakumba wananchi. Kauli hizi zinajiri wakati sekta ya muziki nchini Uganda inaendelea kupanuka kibiashara, lakini changamoto za udhibiti wa kisiasa na mashindano ya kifedha kati ya wasanii na serikali zikibaki kuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wake.

Read More
 Msanii Chino Aomba Maombi Baada ya Kuugua Sana

Msanii Chino Aomba Maombi Baada ya Kuugua Sana

Msanii maarufu wa muziki anayefahamika kwa jina la Chino amewatia mashaka mashabiki wake baada ya kutoa taarifa ya kusikitisha kwamba anaumwa sana na kwa sasa anahitaji maombi kutoka kwa watu wote. Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Chino hakufafanua kwa undani kuhusu hali yake ya kiafya, lakini alieleza kuwa anapitia kipindi kigumu na moyo wake unahitaji faraja na sala kutoka kwa wale wanaomjali. Taarifa hiyo imezua hisia tofauti miongoni mwa mashabiki na watu wa karibu, huku wengi wakimiminika kumtakia ahueni ya haraka na kumtia moyo kupitia maoni na ujumbe wa matumaini. Mashabiki na wapenzi wa muziki wake wameombwa kuungana kwa sala na dua ili Chino apate nafuu haraka na kurejea tena katika hali yake ya kawaida. Tunaendelea kumtakia Chino uponyaji wa haraka na nguvu katika kipindi hiki kigumu

Read More
 Mchekeshaji Arnold Saviour Akwama Kuhudhuria Tamasha la Kikwetu Uholanzi

Mchekeshaji Arnold Saviour Akwama Kuhudhuria Tamasha la Kikwetu Uholanzi

Mchekeshaji maarufu wa Kenya Arnold Saviour hatoweza kushiriki kwenye Tamasha la Kikwetu linalotarajiwa kufanyika nchini Uholanzi baada ya matatizo ya kupata visa kuzima safari yake. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa menejimenti yake, maandalizi yote ya safari yalikuwa yamekamilika, ikiwemo mipangilio ya usafiri na ratiba ya burudani, lakini changamoto za dakika za mwisho katika mchakato wa kupata visa zilipelekea kushindikana kwake kusafiri. Timu yake imesikitishwa na hali hiyo, ikibainisha kuwa pigo hilo si tu linamnyima Saviour nafasi ya kuiwakilisha Kenya kwenye jukwaa la kimataifa, bali pia linaathiri umaarufu na mwonekano wa vipaji vya wasanii wa ndani nje ya nchi. Wameitaka serikali, wadhamini na mashirika yanayohusika na utoaji wa visa kurahisisha taratibu za usafiri kwa wasanii ili kuepusha changamoto kama hizi siku zijazo. Tamasha la Kikwetu ni tukio kubwa linalokutanisha wasanii, wanamuziki na mabalozi wa tamaduni kutoka barani Afrika kwa ajili ya kusherehekea muziki, sanaa na urithi wa kitamaduni. Kukosekana kwa Arnold Saviour hakika kutaacha pengo kubwa kwa mashabiki waliokuwa na hamu ya kumuona akitoa ucheshi wake wa kipekee jukwaani. Hata hivyo, menejimenti yake imewahakikishia mashabiki kuwa Saviour ataendelea kufanyia kazi miradi mipya nchini huku wakitafuta njia mbadala za kumpa nafasi ya kuunganishwa na mashabiki wake wa kimataifa.

Read More
 Akothee Alazwa Hospitalini Baada ya Kuteseka kwa Miezi Miwili

Akothee Alazwa Hospitalini Baada ya Kuteseka kwa Miezi Miwili

Mwanamuziki na mfanyibiashara maarufu nchini, Esther Akoth maarufu kama Akothee, amefichua kuwa amekuwa akisumbuliwa na maumivu makali kwa zaidi ya miezi miwili na hatimaye amelazwa hospitalini tangu Jumatatu wiki hii. Kupitia waraka mrefu kwenye Instagram, Akothee alieleza kuwa maisha yake yamekuwa ya faragha kiasi kwamba mashabiki wake hawakujua hali yake ya kiafya hadi alipoamua kufunguka. Alisema alijisukuma kupita kiasi licha ya kubeba maumivu kwa zaidi ya miezi miwili. Shida hiyo ilijitokeza zaidi wakati wa mtihani wa pili ambapo ghafla akili yake iliganda, karatasi ya mtihani ikaonekana kumlemea na akaanza kuhisi kichefuchefu. Akiwa Homa Bay, alikiri kuwa alitegemea dawa za kupunguza maumivu na za kulegeza misuli ili kuendelea na majukumu yake, akiwemo kumalizia ratiba aliyokuwa ameahidi mashabiki wake. Hata hivyo, alipata shambulio jingine kali wakati alipotarajia kuruhusiwa kuondoka hospitalini, hali iliyomlazimu kuendelea kupata uangalizi wa karibu. Ujumbe wake umeonyesha ni kwa namna gani alijitolea kukamilisha majukumu yake licha ya hali ngumu ya kiafya, jambo lililoibua mjadala mkubwa kuhusu shinikizo la kazi na athari zake kwa wasanii na viongozi wa kijamii. Mashabiki wake wamejitokeza kwa wingi kumtakia nafuu ya haraka, huku wakimsifu kwa ujasiri wa kuendelea kusimama imara licha ya changamoto alizopitia.

Read More
 Bahati Amchana Fred Arocho Kufuatia Sakata la Mchango kwa Harambee Stars

Bahati Amchana Fred Arocho Kufuatia Sakata la Mchango kwa Harambee Stars

Msanii aliyegeukia siasa, Bahati, amemtolea uvivu bila huruma mtangazaji wa Radio 47, Fred Arocho, kufuatia kauli za kumkosoa kwa kuchelewa kutimiza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni moja kwa Harambee Stars. Kupitia Instagram, Bahati amejigamba kuwa ana uwezo mkubwa kifedha na hata akitaka anaweza kumpigia mmiliki wa Radio 47 sasa hivi na kununua kituo hicho. Amesema pia yuko tayari kumweka mke wake, Diana Marua, kama boss wa kituo hicho cha redio ambacho Arocho hufanyia kazi, akisisitiza kwamba pesa kwake si tatizo. Haikuishia hapo amejinasibu kuhusu utajiri wake, kwa kusema kwamba kwa wiki moja hutumia shilingi milioni tatu, na hata baada ya mwaka mmoja bila kutoa wimbo mpya bado anaendelea kustawi kifedha. Hitmaker huyo wa Pete yangu, amefafanua kuwa kuchelewa kutoa mchango wake hakumaanishi hana nia ya kusaidia. Ameeleza kwamba alikuwa amejiandaa kwa muda wa wiki nzima kuandaa sherehe kubwa ya kuzaliwa kwa mtoto wake, hafla ambayo hakutaka kuiahirisha kwa ajili ya kutoa mchango huo. Hata hivyo, Bahati amelalamika kwamba hata pale alipokuwa tayari kuwasilisha mchango wake kwa timu ya taifa, hakukuwa na mtu aliyejitokeza rasmi kupokea, akimlaumu kiungo wa zamani wa Harambee Stars McDonald Mariga kwa kutopokea simu zake. Kauli ya Bahati inakuja wiki moja baada ya, Arocho kueleza kutoridhishwa na ahadi ya msanii huyo kwa timu ya taifa akisema kwamba mashabiki na wachezaji wa Harambee Stars walikuwa wakisubiri kwa matumaini makubwa msaada huo, na kuchelewa kwake kumeonekana kama njia ya kujitafutia kiki.

Read More
 DJ Shiti Asababisha Vicheko kwa Video ya Maombi ya Sheng kwa Patelo

DJ Shiti Asababisha Vicheko kwa Video ya Maombi ya Sheng kwa Patelo

Mchekeshaji maarufu DJ Shiti ameibua kicheko mitandaoni baada ya kujitokeza kwa njia ya ucheshi kumuombea VJ Patelo, kufuatia tetesi kwamba ndoa yake na mkewe Dee imeingiwa na ukungu. Kupitia video ambayo kwa sasa inasambaa, DJ Shiti amesikika akitumia lugha tata ya Sheng kuomba mikosi imuondokee Patelo. Lugha hiyo, iliyojaa maneno ya ucheshi na misemo isiyoeleweka kirahisi, imewafanya mashabiki wengi kucheka huku wengine wakisema maombi hayo ndiyo dawa ya jini mkata kamba linalodaiwa kuingia kwenye ndoa ya Patelo. “Baba nakabidhi Patelo mikono mwako, chude ngenje, chude ngenje siku zombotote ngezo zikuje nyingi. Ngezo zikuje kama zombotote apate shagla kama zombotote. Nakataa maroho ya chang’ili nakataa roho ya black devil. Nambariki na roho ya Captain Morgan siku zombotote. Gota hatujawahi bugunda!!”, Alisikika akisema kwenye video inayosambaa mtandaoni. Video ya DJ Shiti imekuja siku chache baada ya ile iliyosambaa ikimuonyesha Dee akimzaba kofi Patelo walipokuwa katika nightclub moja jijini Nairobi, tukio lililoibua tetesi kwamba ndoa yao inakumbwa na changamoto. Hata hivyo, VJ Patelo mwenyewe amekanusha vikali madai hayo, akisisitiza kuwa ndoa yake iko imara na haina misukosuko. Akiwa amekasirishwa na tetesi hizo, Patelo aliwaambia wakosoaji wake wajishughulishe na maisha yao badala ya kufuatilia mambo ya kifamilia yake. Kauli ya Patelo imeonekana kama onyo kali kwa wanaoendeleza uvumi mitandaoni, huku DJ Shiti akigeuza sakata hilo kuwa kichekesho kwa maombi yake ya Sheng ambayo yamewachekesha wengi.

Read More
 Zuchu Apewa Heshima Kutumbuiza Kwenye Fainali za CHAN 2025 Kenya

Zuchu Apewa Heshima Kutumbuiza Kwenye Fainali za CHAN 2025 Kenya

Msanii maarufu wa Tanzania, Zuchu, ameteuliwa kuwa msanii kinara atakayetumbuiza kwenye sherehe za kufunga mashindano ya CHAN 2025 yatakayofanyika wikiendi hii katika Uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani jijini Nairobi. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zuchu alieleza furaha yake akitangaza kuwa atakuwa msanii mkuu wa burudani kwenye fainali hizo, hatua ambayo imepokelewa kwa shangwe na mashabiki wake barani Afrika na kwingineko. Tangazo hilo pia liliibua pongezi kutoka kwa mastaa wa muziki, akiwemo Diamond Platnumz, ambaye alionyesha kufurahishwa na mafanikio ya mpenzi wake na kueleza kuwa hatua hiyo ni kubwa na inamfanya ajivunie zaidi. Sherehe za kufunga mashindano zinatarajiwa kuwa na burudani ya kipekee kabla ya mchezo wa fainali utakaozikutanisha timu za Morocco na Madagascar Jumamosi, tarehe 30 Agosti 2025, ambapo mshindi atavikwa taji la ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Read More