Eliud Kipchoge Kukutana Tena na Kenenisa Bekele Kwenye Marathoni ya New York

Eliud Kipchoge Kukutana Tena na Kenenisa Bekele Kwenye Marathoni ya New York

Mwanariadha mashuhuri wa Kenya, Eliud Kipchoge, anatarajiwa kukutana tena na mpinzani wake wa muda mrefu Kenenisa Bekele kutoka Ethiopia kwenye mbio za Marathoni za Jijini New York zitakazofanyika tarehe 2 Novemba mwaka huu. Bekele, ambaye ni mmoja wa wanariadha bora wa mbio za masafa marefu katika historia, amejumuishwa kwenye orodha ya washiriki akichukua nafasi ya bingwa wa mwaka 2022, Evans Chebet. Kipchoge na Bekele wamewahi kukutana mara tano kwenye mbio za marathoni, na safari hii inatarajiwa kuwasha upya ushindani mkali kati yao. Kwa upande wa Kipchoge, hii itakuwa mara yake ya kwanza kushiriki katika marathoni ya New York, huku Bekele akirejea baada ya mbio zake za mwisho mwaka 2021, ambapo alimaliza katika nafasi ya sita. Katika michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka 2024, Bekele alimaliza wa 39 kwa muda wa saa mbili dakika kumi na mbili na sekunde ishirini na nne, ilihali Kipchoge hakuweza kumaliza kutokana na jeraha la nyonga. Mashindano haya yanatarajiwa kuvutia macho ya mashabiki wa riadha duniani kote, huku wawili hao wakipimana ubabe kwenye jiji la New York. Kwa Eliud Kipchoge, mbio hizi ni sehemu ya azma yake ya kushiriki mbio zote saba kuu za Abbott World Marathon Majors.

Read More
 Ringtone Apatwa na Kizaazaa Baada ya Tiktoker Kuvuruga Huduma ya Mahubiri Mtandaoni

Ringtone Apatwa na Kizaazaa Baada ya Tiktoker Kuvuruga Huduma ya Mahubiri Mtandaoni

Msanii wa nyimbo za injili, Ringtone Apoko, amejipata katika hali ya sintofahamu baada ya tukio lisilo la kawaida kutokea wakati wa huduma yake ya mahubiri kupitia TikTok Live. Kwa mujibu wa video iliyosambaa mtandaoni, msanii huyo alikuwa akihubiri na kuwasihi wafuasi wake kumrudia Mwenyezi Mungu, wakati ghafla Tiktoker mmoja mrembo aliingilia kati matangazo hayo ya moja kwa moja na kuanza kumtuhumu Ringtone kwa kupotosha umma. Hata hivyo, hali ilibadilika zaidi wakati mrembo huyo alianza kumtaka kimahaba msanii huyo, akitumia lugha ya matusi na maneno yasiyokuwa na staha, jambo lililowashangaza watazamaji wa kipindi hicho. Ringtone, ambaye alionekana akijaribu kumtuliza mrembo huyo kwa busara, alilazimika kusitisha huduma hiyo ya moja kwa moja kutokana na mazungumzo hayo ya aibu ambayo yalikuwa yakimvunjia heshima mbele ya mashabiki wake.

Read More
 Msanii Dyana Cods Afichua Idadi ya Ngoma Kwenye Albamu Yake Mpya

Msanii Dyana Cods Afichua Idadi ya Ngoma Kwenye Albamu Yake Mpya

Msanii kutoka nchini Kenya, Dyana Cods, ameweka wazi idadi ya nyimbo zitakazopatikana kwenye albamu yake mpya inayotarajiwa kuingia sokoni hivi karibuni. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dyana amewajulisha mashabiki wake kuhusu ujio wa albamu hiyo, akisema kuwa itakuwa na ngoma 16 za moto, huku akimalizia chapisho lake kwa hashtag #GhettoGirl, ikionekana kuwa huenda ndilo jina la albamu hiyo. Ingawa hajafichua majina ya nyimbo hizo wala wasanii aliowashirikisha, Dyana amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula kuipokea rasmi albamu hiyo ambayo inaashiria hatua mpya katika safari yake ya muziki. Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, Dyana Cods tayari ana albamu kadhaa zilizotolewa miaka ya nyuma zikiwemo Late Night Kneeler (2019), Thank Me Later (2022), River Lake Nilote (2023), na Rong Manners (2024). Albamu yake mpya itakuwa ya tano katika msururu wa kazi zake, ikionyesha mwendelezo wa ubunifu na ukuaji wake katika tasnia ya muziki nchini Kenya.

Read More
 Msanii Pipi Jojo Aangua Kilio Baada ya Chief Godlove Kumkimbia

Msanii Pipi Jojo Aangua Kilio Baada ya Chief Godlove Kumkimbia

Msanii wa Chief Godlove, anayefahamika kwa jina la Pipi jojo, ameangua kilio hadharani baada ya kugundua kwamba ataanza ziara yake ya vyombo vya habari nchini Kenya bila ushirika wa meneja wake huyo maarufu. Kupitia video inayosambaa mtandaoni, Pipijojo ameonekana akibubujikwa na machozi huku Chief Godlove akimfariji na kumtia moyo kabla ya safari yake. Katika ujumbe aliouchapisha kupitia ukurasa wake wa Instagram, Chief Godlove amesema kuwa binti yake Pipi Jojo amepata mwaliko wa kwenda kwenye media tour nchini Kenya, na kwamba alitarajia kumsindikiza mwenyewe lakini alishindwa kutokana na majukumu ya kikazi. Ziara hiyo inatarajiwa kuanza wiki ijayo, ambapo Pipi jojo atazuru vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini Kenya kwa ajili ya kutangaza miradi yake mipya ya muziki. Ziara ya Pipijojo nchini Kenya inatazamiwa kuwa hatua muhimu katika kukuza jina lake kimataifa na kuimarisha ushawishi wa muziki wa lebo ya Chief Godlove katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Read More
 Justina Syokau Aonyesha Upendo kwa Hayati Raila Odinga kwa Kunyoa Nywele Zake

Justina Syokau Aonyesha Upendo kwa Hayati Raila Odinga kwa Kunyoa Nywele Zake

Mwanamuziki wa injili kutoka nchini Kenya, Justina Syokau, ameonyesha ishara ya heshima na upendo kwa hayati Raila Odinga kwa kunyoa nywele zake zote. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Syokau aMEposti video akiwa saloon akinyolewa nywele na kueleza kuwa aliamua kufanya hivyo ili kumheshimu na kumuomboleza Baba Raila Odinga. Lakini pia amebainisha kuwa amerekodi wimbo maalum wa kumbukumbu kama sehemu ya heshima yake kwa kiongozi huyo mashuhuri. Hata hivyo Syokau amesema kitendo hicho ni njia yake ya kuonyesha upendo na kuthamini mchango mkubwa wa kisiasa na kijamii alioutoa Raila kwa taifa la Kenya.

Read More
 Yemi Alade Afichua Aliwahi Kudanganya Umri Wake kwa Miaka Mitatu

Yemi Alade Afichua Aliwahi Kudanganya Umri Wake kwa Miaka Mitatu

Mwanamuziki kutoka nchini Nigeria, Yemi Alade, amefichua kuwa aliwahi kudanganya umri wake kwa miaka mitatu, akidai ana miaka 22 ilhali kwa wakati huo alikuwa na miaka 25. Katika mahojiano ya hivi karibuni, Yemi Alade ameeleza kuwa aliamua kufanya hivyo kutokana na shinikizo la kijamii na tasnia ya muziki, ambayo mara nyingi huwapa nafasi zaidi wasanii wachanga. Kitendo hicho, amesema, kilimfanya apate msongo wa mawazo kutokana na ugumu wa kuishi na uongo huo na kutokukubali ukweli kuhusu umri wake halisi. Msanii huyo wa wimbo waa Johnny amefafanua kuwa uamuzi huo ulisababisha apoteze kujiamini na kukosa amani kwa muda mrefu, kwani kila mara aliishi kwa hofu ya ukweli wake kufichuka. Hata hivyo, amesema ameweza kujifunza umuhimu wa kukubali umri na safari yake binafsi, akisisitiza kuwa huwezi kudanganya muda wala kujificha nyuma ya umri mwingine. Yemi Alade, ambaye amekuwa mmoja wa nyota wakubwa wa muziki wa Afro-pop barani Afrika, sasa anasema anathamini zaidi ukweli na anawahimiza wasanii wengine kuwa wa kweli kuhusu maisha yao binafsi.

Read More
 Msanii wa Uganda Olisha M Afariki Dunia Wakati wa Kujifungua

Msanii wa Uganda Olisha M Afariki Dunia Wakati wa Kujifungua

Tasnia ya muziki nchini Uganda imo kwenye majonzi kufuatia kifo cha mwanamuziki Olisha M, aliyeripotiwa kufariki jana jioni wakati wa kujifungua katika hospitali moja maarufu jijini Kampala. Olisha M, anayejulikana kwa vibao vyake kama Katambala, Super Love, na Gwenjagala, alikuwa mmoja wa wanamuziki chipukizi waliokuwa wakifanya vyema kwenye muziki wa kizazi kipya nchini humo. Habari za kifo chake zimeutikisa ulimwengu wa burudani na kuwahuzunisha mashabiki wake ndani na nje ya Uganda. Mwanamuziki huyo, ambaye mwaka jana alifanikisha sherehe ya kumtambulisha rasmi mchumba wake katika hafla iliyovutia umma, aliripotiwa kuwa katika hali nzuri ya kiafya kabla ya tukio hilo la kusikitisha kutokea. Tangu taarifa za kifo chake kutangazwa, mitandao ya kijamii imefurika jumbe za rambirambi kutoka kwa mashabiki, wasanii wenzake, na wadau wa muziki waliomkumbuka kwa sauti yake na mchango wake katika sanaa.

Read More
 Kenya yazidi kusonga mbele kuelekea Kombe la Afrika la Wanawake

Kenya yazidi kusonga mbele kuelekea Kombe la Afrika la Wanawake

timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Gambia katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya mwisho ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika la Wanawake 2026. Mechi hiyo ilichezwa jana kwenye Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, Nairobi. Mechi ya mkondo wa pili itafanyika Jumanne ijayo kwenye Stade Lat Dior jijini Thies, Senegal, kwani Gambia haina uwanja unaokidhi viwango vya CAF. Mshindi wa jumla wa mechi hiyo atapata tiketi ya kufuzu WAFCON 2026, itakayofanyika Morocco kuanzia 17 Machi hadi 3 Aprili mwaka ujao. Rais William Samoei Ruto amewazawadia Starlets shilingi milioni 5 kama motisha ya ushindi huu. Aidha, Rais amewaahidi timu hiyo shilingi milioni 2.5 kwa sare, shilingi milioni 1 kwa kila mchezaji iwapo watashinda kufuzu WAFCON, na shilingi 500,000 kwa kila mchezaji iwapo watafuzu kwa sare. Huu ni ushindi muhimu kwa Starlets, wakijipanga kuendeleza hadhi ya soka la wanawake nchini Kenya na kuendeleza matumaini ya kufuzu fainali za WAFCON mwaka ujao.”

Read More
 Instagram yazindua kipengele kipya cha kuchora ndani ya DM

Instagram yazindua kipengele kipya cha kuchora ndani ya DM

Kampuni ya Instagram imeweka mabadiliko mapya katika sehemu ya Direct Messages (DM), ambapo sasa watumiaji wote wanaweza kuchora moja kwa moja kwenye skrini ya mazungumzo. Kupitia mfumo huu mpya, mtumiaji anaweza kuchora au kuandika kwa mkono katika sehemu yoyote ya skrini ya DM, na mtu anayewasiliana naye ataweza kuona michoro hiyo papo kwa papo, bila kuchelewa. Kipengele hiki kipya kinapatikana kupitia alama ya (+) iliyopo chini ya skrini ya mazungumzo. Baada ya kubonyeza alama hiyo, mtumiaji ataona chaguo jipya lenye jina “Draw”, ambalo linamruhusu kuchora au kuandika alivyotaka moja kwa moja ndani ya DM. Instagram imesema maboresho haya yamelenga kuongeza ubunifu na njia za kujieleza kwa watumiaji wake, sambamba na kuboresha uzoefu wa mawasiliano binafsi. Kipengele hiki kinatarajiwa kuwafikia watumiaji wote duniani katika hatua za awali za masasisho mapya ya programu hiyo.

Read More
 Otile Brown Atangaza Wimbo wa Kumbukumbu kwa Baba Raila Odinga

Otile Brown Atangaza Wimbo wa Kumbukumbu kwa Baba Raila Odinga

Staa wa muziki wa Bongo RnB, Otile Brown, ametangaza ujio wa wimbo mpya wa kumbukumbu kwa Baba Raila Odinga, siku chache tu baada ya kiongozi huyo kuzikwa. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Otile amesema kuwa mwezi Novemba atatoa wimbo ulio karibu sana na moyo wake, akisema ni wimbo wa heshima na kumbukumbu kwa Raila na kwa wote waliopoteza wapendwa wao. Msanii huyo amesisitiza kuwa baadhi ya matukio ni zenye nguvu kiasi kwamba haziwezi kunyamaziwa, na kwamba muziki wake utakuwa njia ya kuenzi maisha na urithi wa Baba. Mashabiki wengi wamepongeza hatua ya Otile Brown wakisema ni njia ya heshima na kumbukumbu kwa kiongozi ambaye amegusa maisha ya Wakenya wengi.

Read More
 KRG The Don Awakosoa Viongozi Kenya Wanaochochea Migawanyiko

KRG The Don Awakosoa Viongozi Kenya Wanaochochea Migawanyiko

Mwanamuziki wa Kenya, KRG The Don, amewakashifu vikali viongozi na wananchi wanaochochea migawanyiko na chuki miongoni mwa Wakenya. Kupitia ujumbe aliouchapisha mitandaoni, KRG amesema kuwa ni aibu kwa viongozi na raia wanaofurahia au kuchangia mgawanyiko wa kitaifa badala ya kuhimiza umoja na mshikamano. Msanii huyo ameeleza kuwa taifa haliwezi kusonga mbele endapo Wakenya wataendelea kugawanyika kwa misingi ya ukabila, dini au chama cha siasa. Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuhubiri amani na maridhiano badala ya kugawanya wananchi kwa maneno na vitendo vya uchochezi. Hata hivyo KRG The Don, amehimiza vijana kutumia nguvu zao katika kujenga amani na kuhamasisha umoja nchini Kenya. Ameongeza kuwa ni wajibu wa kila Mkenya kulinda utu na heshima ya taifa kwa kuepuka mijadala ya chuki na mizozo ya kisiasa inayoharibu umoja wa nchi.

Read More
 Eric Omondi Asema Kuzaliwa kwa Kenya Mpya Ni Jambo Lisilozuilika

Eric Omondi Asema Kuzaliwa kwa Kenya Mpya Ni Jambo Lisilozuilika

Mchekeshaji na mwanaharakati wa kijamii Eric Omondi amesema kuwa kuzaliwa kwa Kenya mpya ni jambo lisiloweza kuzuilika, akieleza kuwa kizazi kipya kinachojitokeza sasa ni cha Wakenya wasioangalia ukabila, bali umoja na mabadiliko. Kupitia ujumbe wake Instagram, Omondi amesema kuwa “The birth of a new Kenya is inevitable”, akisisitiza kuwa taifa la Kenya linaingia katika kipindi kipya cha mageuzi ya kijamii na kisiasa ambacho kitavunja ukabila, ufisadi, na tamaa ya mali. Eric anaamini kuwa kizazi kipya cha Wakenya kimeamka na kiko tayari kupigania taifa lenye haki, usawa na uwajibikaji. Kwa mujibu wake, mabadiliko haya hayatategemea wanasiasa wa jadi, bali vijana na raia wa kawaida wanaotaka kuona Kenya yenye amani na maendeleo. Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Omondi kuzindua kampeni maalum ya kuhamasisha vijana katika vyuo vikuu kujisajili kama wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Kampeni hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika maamuzi ya kisiasa na kuhakikisha sauti yao inasikika kwenye mustakabali wa taifa.

Read More