YouTube Yafungua Mlango Mpya wa Ubunifu Kupitia Akili Bandia
Kampuni ya YouTube imetangaza kuanzisha rasmi matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) inayoitwa Veo katika programu na tovuti zake, hatua inayolenga kurahisisha utengenezaji wa video kwa watumiaji wake duniani kote. Kupitia mfumo huu, watumiaji wataweza kutengeneza video kwa kutumia maelezo ya maandishi tu, bila kuhitaji ujuzi wa kina katika uhariri wa video au vifaa maalum vya kitaalamu. Veo ni teknolojia ya hali ya juu inayoweza kutafsiri maelezo mafupi (text prompts) na kuyabadilisha kuwa video za ubora wa juu. Kwa mfano, mtumiaji anaweza kuandika sentensi kama picha ya jua linapotua baharini na AI hiyo kutengeneza video inayolingana na maelezo hayo. YouTube imeeleza kuwa teknolojia hii inalenga kuwasaidia wabunifu wa maudhui wazo likitoka kichwani moja kwa moja hadi kuwa video halisi. Mbali na kutengeneza video mpya, mfumo wa Veo pia utawapa watumiaji uwezo wa kuhariri maudhui yao kwa kutumia sauti au maandishi, pamoja na kupokea mapendekezo ya uhariri kutoka kwa AI hiyo. Hii ni sehemu ya juhudi za YouTube kuendeleza ubunifu na kurahisisha kazi ya wabunifu wa maudhui wa kizazi kipya, bila kuwabana kwa gharama au ujuzi wa kiufundi. Kwa sasa, YouTube imesema mfumo huu utaanza kwa watumiaji wachache walioteuliwa katika kipindi cha majaribio kabla ya kusambazwa kwa watumiaji wote duniani. Wakati wadau wa teknolojia na ubunifu wakipokea habari hii kwa furaha, pia kumekuwepo na mjadala kuhusu nafasi ya binadamu katika uumbaji wa maudhui. Hata hivyo, YouTube imesisitiza kuwa lengo la Veo ni kuongeza ubunifu wa binadamu, si kuubadilisha.
Read More