
Mwanamuziki maarufu wa Marekani, Belcalis Almanzar, Maarufu kama Cardi B, amefichua kuwa mzazi mwenzake na rapa wa kundi la Migos, Offset, hajatoa msaada wowote wa kifedha kwa watoto wao kwa kipindi cha miezi minane.
Akiwa anajibu kauli ya Offset aliyoitoa katika mahojiano na The Breakfast Club, Cardi B alikanusha vikali madai kwamba yeye ni mzazi asiyejali, akieleza kuwa ndiye anayebeba majukumu yote ya kifamilia. Cardi alisema kuwa amekuwa akitumia hadi dola 50,000 kwa mwezi kwa ajili ya watoto wao, na kumshutumu Offset kwa kushindwa kuwajibika kama baba.
“Natumia dola elfu hamsini ($50,000) kila mwezi kwa ajili ya watoto wetu, Kutoka kwenye ada za shule, huduma za afya, chakula, usafiri, hadi walinzi binafsi. Mimi ndiye nafanya yote. Mtu aseme mimi ni deadbeat? Hapana.”, Alisema Cardi B kwa hasira.
Cardi B pia alionesha wasiwasi kuhusu hali ya kiakili ya Offset, akimtaka atafute msaada badala ya kueneza tuhuma za uongo dhidi yake mitandaoni.
“Nakupa pole na nafasi kwa sababu najua hauko sawa kiakili. Lakini usitumie hilo kunivunjia heshima mbele ya watoto wetu na hadhira ya dunia nzima,” aliongeza.
Mgogoro huo umeibua hisia kali mitandaoni. Mashabiki wa Cardi B wamemsifu kwa uwazi wake na kujitolea kama mama, huku baadhi ya wafuasi wa Offset wakimtetea na kueleza kuwa anaweza kuwa anashughulika na changamoto za kiakili au presha kutoka kwa timu yake ya kisheria.
Kauli hiyo ya Cardi B inajibu mahojiano ya hivi karibuni ambayo Offset alifanya na kipindi maarufu cha The Breakfast Club, ambapo alieleza kuwa mawakili wake walimshauri kuomba msaada wa kifedha kutoka kwa Cardi kama mkakati wa kisheria kwenye mchakato wa talaka yao. Offset alidai kuwa Cardi alitaka kila kitu katika mgawanyo wa mali, na kwamba maombi yake ni sehemu tu ya kujilinda katika taratibu za mahakama.
Wawili hao, waliowana mwaka 2017, wamekuwa kwenye uhusiano wa uliojaa migogoro, na sasa wapo kwenye hatua za mwisho kukamilisha talaka yao. Wana watoto wawili pamoja Kulture Kiari na Wave Set.