
Mfanyabiashara na mwanasosholaiti maarufu kutoka Kenya, Huddah Monroe, amezua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kutoa kauli yenye utata kuhusu wanaume wa kizazi cha Gen Z. Kupitia mitandao ya kijamii, Huddah alisema kuwa wanaume wa kizazi hiki wamekosa ujasiri wa kutangamana na wanawake na kuanzisha mazungumzo, tofauti kabisa na enzi za Millennials.
Huddah alieleza kushangazwa na tabia ya wanaume wa kizazi cha Gen Z ambao, kwa mtazamo wake, huonekana kuogopa au kutojihusisha moja kwa moja na wanawake katika mazingira ya kijamii.
“Navaa ninja yangu na kwenda sehemu za kijamii kwa ajili ya utafiti wangu tu, maana sina ninayemtaka huko. Lakini wanaume hawakaribii wanawake,” aliandika Huddah.
Huddah aliendelea kueleza kuwa hali hiyo imemfanya awahurumie wanaume wa kizazi hiki kwa sababu mawasiliano ya ana kwa ana yamepungua sana. Kwa maoni yake, kizazi cha sasa kinaonekana kuwa na uwoga au labda kimezidiwa na matumizi ya mitandao ya kijamii, kiasi cha kushindwa kuwa na ujasiri wa kawaida wa kuanzisha mazungumzo.
“Millennials walikuwa na game. Gen Z wanaonekana kama wamekata tamaa. Wengine wakijaribu, mazungumzo yao hayana ladha wala mvuto,” aliongeza.
Kauli hii imechochea maoni mbalimbali, huku baadhi ya mashabiki wakimpongeza kwa kusema anasema ukweli mchungu. Wengine wamehusisha hali hiyo na mabadiliko ya kijamii, hofu ya kukataliwa, au ongezeko la mtazamo hasi dhidi ya wanaume wanaowakaribia wanawake bila mwaliko.
Huddah, ambaye ana sauti kubwa mitandaoni kuhusu masuala ya kijamii, anasema hali hii inaweza kuwa ishara ya matatizo makubwa zaidi katika namna watu wa kizazi kipya wanavyojenga mahusiano.