Entertainment

Jux Atoa EP Maalum Kuelezea Safari Yake ya Mapenzi na Mkewe Priscy

Jux Atoa EP Maalum Kuelezea Safari Yake ya Mapenzi na Mkewe Priscy

Msanii nyota wa Bongo Fleva, Juma Jux, ameachia rasmi kazi yake mpya ya muziki, EP iitwayo “A Day To Remember”, kama kumbukizi maalum ya ndoa yake na mkewe mpendwa, Priscy. Kupitia mitandao ya kijamii, Jux ameeleza kuwa mradi huu si kazi ya kawaida, bali ni simulizi ya maisha yao ya upendo, kuanzia mwanzo wa safari yao ya mahaba hadi furaha waliyonayo sasa kama wanandoa.

EP hiyo imejaa hisia, utamaduni na usanii wa hali ya juu, ikiwa imeshirikisha mastaa wawili wakubwa: Phyno kutoka Nigeria na D Voice kutoka Tanzania. Jux ameamua kuunganisha ladha ya Afrika Mashariki na Magharibi ili kuwasilisha ujumbe wa upendo unaovuka mipaka ya lugha na mataifa.

Kati ya watayarishaji walioweka mikono yao kwenye kazi hii ni S2kizzy, Foxx Made It, na Aykbeats, huku kazi ya mixing na mastering ikifanywa na Lizer Classic, jina kubwa katika ubora wa sauti Afrika.

Katika ujumbe wake, Jux hakusita kumshukuru mkewe Priscy kwa kuwa chanzo cha msukumo wa EP hii, pamoja na familia yake, timu nzima ya wasanii na wahusika waliounga mkono kazi hiyo, na mashabiki waliomfuatilia kwa miaka mingi. Amesisitiza kuwa baada ya harusi yao rasmi, atatoa wimbo wa kipekee kama zawadi ya kufunga sura hii mpya ya maisha.

EP “A Day To Remember” itapatikana kuanzia usiku wa leo kwenye majukwaa yote ya kidijitali ya kusikiliza muziki. Mashabiki tayari wameonyesha hamasa kubwa, wakisubiri kwa shauku kusikia mchanganyiko wa upendo na sanaa katika kazi hii ya kipekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *