
Rapa maarufu wa Kenya, Khaligraph Jones, amefichua safari yake ya kupunguza uzito, akisema kuwa ameweza kupunguza kilo 22 ndani ya miezi mitatu pekee.
Akiweka wazi safari yake ya afya kwenye mahojiano ya hivi karibuni, Khaligraph alieleza kuwa awali alikuwa na uzito wa 137 kg, lakini sasa ana uzito wa 115 kg, hatua aliyofikia kwa kutumia mbinu ya intermittent fasting (kula kwa mpangilio wa muda) pamoja na mazoezi ya mwili.
“Nilikua nakula ngwashe, maji na apple,” alisema rapa huyo, akionyesha kuwa mlo wake ulikuwa mwepesi lakini wenye afya.
Katika mahojiano, Khaligraph pia alimpongeza mwanamitandao maarufu nchini Pritty Vishy kwa jitihada zake za kupunguza uzito, akisema kuwa alihamasishwa na kujitolea kwake, hasa alipokuwa akifanya mazoezi pamoja na mkewe.
“Vishy alikua anajitahidi sana. Ilikua motisha pia kwangu,” alisema.
Aidha, Khaligraph amepuuzilia mbali madai yanayosambaa mtandaoni kuwa Pritty Vishy hutumia dawa kupunguza mwili wake. Alisisitiza kuwa madai hayo hayana msingi na kwamba mafanikio ya Vishy yanatokana na bidii na nidhamu ya hali ya juu.
Mashabiki wengi wamepongeza uamuzi wa Khaligraph wa kuchukua hatua za kuboresha afya yake na kuonyesha mfano kwa wengine kuwa inawezekana kupunguza uzito kwa njia salama na za asili.