Gossip

Malcom Afichua Siri ya Sakata la Mulamwah na Ruth K

Malcom Afichua Siri ya Sakata la Mulamwah na Ruth K

Mwanamtandao maarufu kwa jina la Malcom amezua mjadala mkali mtandaoni baada ya kudai kuwa mchekeshaji Mulamwah na mama ya mtoto wake Ruth K wanalipwa makusudi ili kuwahadaa Wakenya na kuwapotosha kutoka kwenye masuala muhimu yanayoathiri nchi kwa sasa.

Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mitandao ya kijamii, Malcom alidai kuwa sakata ya mapenzi kati ya Mulamwah na Ruth K, ambayo imekuwa gumzo mtandaoni kwa wiki kadhaa sasa, si ya kweli bali ni maigizo yaliyopangwa ili kuvuruga akili za raia.

 “Ni kama kuna watu wanawalipa hawa wasanii kufanya hizi drama ili Wakenya wasifikirie kuhusu shida zao. Mnatupumbaza na mapenzi ya watu wawili ilhali nchi inateketea,” alisema Malcom.

Kauli hiyo imezua maoni tofauti kutoka kwa wafuasi wake na watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii. Baadhi waliunga mkono madai hayo wakisema kuna ushahidi wa wazi kwamba wasanii wengi wanatumiwa kama chombo cha kupunguza makali ya ukosoaji dhidi ya serikali, huku wengine wakimtaka Malcom awasilishe ushahidi wa madai hayo badala ya kueneza tuhuma zisizo na msingi.

Mzozo kati ya Mulamwah na Ruth K umeendelea kutawala vichwa vya habari, huku wawili hao wakitupiana lawama hadharani kuhusu sababu za kuachana kwao. Hata hivyo, kauli ya Malcom imeongeza mtazamo mpya kuhusu kinachoendelea nyuma ya pazia.

Wakati huo huo, baadhi ya wadadisi wa masuala ya kijamii wameshauri umma kuwa makini na kile wanachokiona mitandaoni, wakisema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa propaganda na mchezo wa kiakili unaoendeshwa kwa makusudi ili kuelekeza umakini wa wananchi mbali na masuala kama vile ongezeko la gharama ya maisha, maandamano ya wanafunzi, na migogoro katika sekta ya afya na elimu.

Hadi kufikia sasa, Mulamwah wala Ruth K hawajajibu hadharani madai hayo mapya kutoka kwa Malcom.