
Msanii mashuhuri wa Kenya, Bien Aime Baraza, ameweka historia kwa kuwa msanii wa kwanza kutoka Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla kuhojiwa katika kipindi maarufu cha The Breakfast Club nchini Marekani. Hatua hii imepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa muziki barani Afrika, ikionekana kama mafanikio makubwa kwa muziki wa ukanda huu.
Katika mahojiano hayo ya kipekee, Bien alifunguka kuhusu maisha yake ya kifamilia, akisisitiza umuhimu wa uwazi katika ndoa yake. Mkali huyo wa bendi ya Sauti Sol, alionyesha kuwa uaminifu na ushirikiano ndio msingi wa mafanikio yao ya kindoa.
“Kwenye nyumba yangu, pesa ni za familia. Mke wangu ana ufikiaji wa pesa zangu zote nami pia nina ufikiaji wa pesa zake zote,” alisema Bien kwa uwazi,
Mbali na maisha ya nyumbani, Bien pia aligusia muziki wa Kenya na alitoa heshima kwa vipaji vya hapa nyumbani kwa kueleza wasanii anaowakubali zaidi.
“Wasanii ninaowapenda sana Kenya ni Nyashinski, Ywaya kutoka kundi la Watendawili, Kodong Klan na Njerae,” alieleza Bien,
Hatua yake ya kuonekana kwenye The Breakfast Club inachukuliwa kama ushindi mkubwa kwa muziki wa Afrika Mashariki na imezidi kuonyesha kuwa wasanii kutoka ukanda huu wana nafasi kubwa kwenye jukwaa la kimataifa. Mashabiki mitandaoni wameonyesha fahari na pongezi, wakimpongeza Bien kwa kulipeperusha vyema bendera ya Kenya kimataifa.