
Malkia wa muziki wa Rap kutoka Marekani Nicki Minaj ameonyesha upendo kwa kizazi kipya cha wasanii katika mahojiano mapya na Vogue Italia. Rapa huyo mwenye mafanikio makubwa alimtaja Sabrina Carpenter kama msanii anayemvutia kwa ubunifu na mvuto wa kipekee, akieleza kuwa aligundua kipaji chake hivi karibuni licha ya Carpenter kuwa kwenye muziki kwa muda.
“Sabrina Carpenter… ni kama pumzi safi ya hewa,” alisema Minaj. “Sikujua kwamba alikuwa kwenye game kwa muda mrefu kiasi hicho nilipoanza kumsikiliza.”
Aidha, alimsifu Billie Eilish kwa ubunifu wake wa kipekee katika muziki wa kisasa. Licha ya kutotajwa rasmi, Eilish anasikika katika utangulizi wa albamu ya Nicki Pink Friday 2, ishara kwamba uhusiano wa kisanii kati yao tayari umeanza kuchipua.
“Napenda kila kitu anachofanya. Ni msanii wa kipekee sana.”, Nicki alisema.
Nicki pia alimpongeza Skeng, msanii wa dancehall kutoka Jamaica, kama mmoja wa wanaoleta ladha tofauti kwenye muziki wa sasa.
Akizungumzia mitandao ya kijamii, Nicki alieleza kuwa ingawa ina athari kubwa katika kujenga majina ya wasanii, bado kipaji halisi hujitokeza hata bila ushawishi wa mtandao.
“Superstar ni superstar, iwe na mitandao ya kijamii au bila.”, Alilisitiza Minaj.
Mashabiki sasa wana matumaini ya kuona mashirikiano ya wazi kati ya Nicki na wasanii hao aliowataja hasa Carpenter, ambaye bado hawajafanya kazi pamoja.