Entertainment

Pallaso Aweka Wazi Msimamo Wake Kuhusu Siasa

Pallaso Aweka Wazi Msimamo Wake Kuhusu Siasa

Msanii maarufu wa muziki nchini Uganda, Pius Mayanja almaarufu Pallaso, amesema kwa sasa hana mpango wa kujiingiza kwenye masuala ya siasa, akisisitiza kuwa bado anajikita kikamilifu katika taaluma yake ya muziki.

Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni, Pallaso alieleza kuwa hajatimiza malengo aliyojiwekea katika muziki, na hivyo anataka kuyakamilisha kabla ya kufikiria kuchukua jukumu lolote jipya katika maisha yake ya kitaaluma.

 “Sihitaji kuingia kwenye siasa kwa sasa. Niko katika harakati za kutimiza ndoto yangu ya muziki, na nataka kuikamilisha kikamilifu kabla ya kufikiria jambo lolote jingine.”

Ingawa hajajitosa rasmi katika siasa, Pallaso alisema anaendelea kutumia muziki wake kama chombo cha kuwasilisha ujumbe wa kijamii na kisiasa. Anaamini kuwa muziki ni jukwaa lenye nguvu kubwa la kufikisha ujumbe, na ndilo eneo analolielewa vyema.

“Siasa ni wito. Binafsi bado sijaupata. Nikihisi moyoni kwamba ni wakati wa kuingia katika siasa, nitafanya hivyo. Lakini kwa sasa, ninaendelea kuwasilisha ujumbe wangu kupitia muziki.”

Kauli ya Pallaso inajiri wakati ambapo baadhi ya wasanii nchini Uganda wameanza kujitosa katika siasa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. Miongoni mwao ni Big Eye na Nina Roz, ambao tayari wametangaza nia ya kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa.

Ingawa Pallaso hana pingamizi kwa wasanii kuingia katika siasa, amesema ataingia katika ulingo huo pale tu atakapohisi kwa dhati kuwa ni wito wake wa kweli kulitumikia taifa. Kwa sasa, anabaki kuwa mmoja wa wasanii wanaotumia kazi zao kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *